Hakuna tena bomoabomoa mita 60 mito ya mijini

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema hakutakuwa na ubomoaji wa nyumba za watu waliojenga karibu na kingo za mito mijini kwa kuwa mito huwa inahama mara kwa mara kila wakati.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Makamba alisema licha ya makosa yaliyofanywa na mipango miji siku za nyuma, kwa sasa ni vigumu kutekeleza sheria ya mazingira inayotaka nyumba hizo zijengwe nje ya mita 60 kutoka mtoni.

“Mita 60 haitakuwapo kwa sababu hamna namna kwenye maeneo ya mijini ukapata uhalisia. Mto unaopita Chalinze ni tofauti na mto unaopita mjini. Sheria lazima iangalie mazingira na watu na uhalisia,” alisema Makamba.

Alisema kwa makosa yaliyofanyika ukipiga mstari wa mita 60 ukabomoa nyumba utabomoa nusu ya Dar es Salaam, iwe ni siasa au siyo siasa. Hivyo, alisema lazima busara itumike.

Akizungumzia Bonde la Msimbazi, Makamba alisema kwa muda mrefu sasa bonde hilo lina utata mkubwa, lakini tayari kuna mradi unaofadhiwa na Benki ya Dunia (WB) unakwenda kumaliza changamoto zote.

“Changamoto zake ni watu kujenga karibu na mto, kwa hiyo taka zinajaa mtoni na mafuriko yakija inakuwa shida kwa watu. Kwa hiyo namna ya kusaidia ni kuwaondoa kwenye mto, lakini kulikuwa na changamoto katika mipango miji tangu zamani kiasi kwamba unapomtoa mtu lakini alikuwa ameshahalalishwa,” alisema.

“Halafu mto unahamahama kiasi kwamba kupata mita 60 inashindikana. Utapiga mstari kwamba hapa ndiyo mwisho, halafu yanapokuja maji mto unahama. Ndiyo maana hakuna haja ya kubomoa kwa sababu utashindwa kabisa kuwaondoa.” Hata hivyo, alisema watu waliojenga katikati ya mto huo wataondolewa.

Kuhusu Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), alisema kuna mabadiliko makubwa yamefanyika ambayo ni pamoja na kulitoa kuwa ‘kijiwe’ kwenda kuwa taasisi ya huduma.

“Nemc ilikuwa kama kijiweni, unakwenda pale unachukua cheti chako unaondoka, usipokuwa unamjua mtu cheti kinacheleweshwa kwa makusudi,” alisema Makamba.

“Katika moja ya kazi ambayo mimi najivunia tangu niteuliwe katika wizara hii ni mabadiliko tuliyofanya Nemc hasa mwaka mmoja uliopita ya kujaribu kuibadilisha kutoka taasisi ya kipolisi na kijiwe kuwa taasisi ya kutoa huduma.”

Alitaja mabadiliko mengine kuwa ni kurekebisha sheria na kanuni ili kuondoa vikwazo kwa wawekezaji.

Alisema, “kwa ujumla wingi wa hizi mamlaka za udhibiti na tozo zimekuwa kero kwa wawekezaji. Sisi tumefanya mambo matatu, kwanza kuharakisha utoaji wa vyeti, sasa hivi unatakiwa upewe cheti cha mazingira. Tunafanya checklist wakati mchakato unaendelea.”

“Halafu tumepunguza sana gharama, sasa hivi EIA (tathmini ya mazingira) tunafanya kwa gharama iliyopo, huko nyuma kufanya EIA ilikuwa chanzo cha mapato, sasa hivi tunafanya kwa gharama inayohusika tu.”