Halima Mdee asimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki, Maadili, Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka alipokuwa akiwasilisha bungeni taarifa ya kamati yake kuhusu shauri dhidi yake la kulidharirisha Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Baada ya kamati ya haki, maadili na madaraka ya bunge kupendekeza mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kusimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya bunge, chombo hicho cha kutunga sheria kimeridhia hoja hiyo na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema mbunge huyo hatahudhuria mkutano wote wa bajeti ulioanza leo hadi Juni 28 pamoja na mkutano wa 16 utakaofanyika Septemba na Oktoba.


Dodoma. Bunge la Tanzania limemsimamisha mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili ya chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuwa bunge ni dhaifu.

Uamuzi huo umefikiwa leo mchana baada ya kamati ya haki, maadili na madaraka ya bunge kutoa mapendekezo yake ikirejea majibu ya Mdee aliyoyatoa alipohojiwa na kamati hiyo.

Katika maelezo yake, Naibu Spika Dk Tulia Ackson amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuwahoji wabunge na kuridhia mbunge huyo kusimamishwa kuhudhuria mikutano hiyo miwili baada ya kujadili mapendekezo hayo ya kamati.

Katika mjadala huo kuhusu uamuzi wa kamati, mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alirudia kauli kuwa bunge ni dhaifu na kujikuta matatani baada ya Dk Tulia kuagiza naye akahojiwe na kamati hiyo kuthibitisha kauli yake.

"Bunge limeazimia kuwa Mdee hatashiriki mkutano huu (wa bajeti)  wa 15 wa bunge na mkutano wa 16 utakaofanyika Septemba na Oktoba, 2019," amesema Dk Tulia.

Awali, mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka amesema wakati wakimuhoji Mdee alikiri kutoa kauli kuwa bunge ni dhaifu.

“Mdee amekiuka masharti ya kifungu 26E cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge kwa kutamka maneno ya kudharau na kudhalilisha bunge. Mdee hii ni mara ya nne kuitwa katika kamati na amewahi kutiwa hatiani mara tatu, kwa shauri hili Mdee amevunja kifungu hiki.”

“Mdee aliwaita wanahabari na kutamka bunge ni dhaifu na akiwa mbele ya kamati hakujutia kauli yake na amekuwa akitoa kauli za namna hii, bunge linaazimia kuwa asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili wa bunge,” amesema Mwakasaka.