Halima Mdee asimulia polisi walivyotawanya mkutano wa Bawacha

Muktasari:

Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesimulia jinsi Jeshi la Polisi wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu lilivyotawanya mkutano wa baraza hilo kwa mabomu ya machozi


Bariadi. Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee amesimulia jinsi Jeshi la Polisi wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu lilivyotawanya mkutano wa baraza hilo kwa mabomu ya machozi.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 13, 2019 Mdee amesema mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Double H ulihudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga inayounda Kanda ya Serengeti ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Mbunge huyo wa Kawe amesema kusambaratishwa kwa kikao hicho siyo tu ni kuvunja sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, bali ni mwendelezo wa polisi kuvibana vyama vya upinzani.

Amesema polisi walipofika eneo hilo waliwataka kuonyesha kibali cha kufanya kikao hicho na walipowaeleza kuwa vikao vya ndani havihitaji vibali ndipo wakabadilisha kauli kwa kudai vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya vikao kwenye kumbi binafsi.

Akizungumza na Mwananchi leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, William Mkonda alithibitisha kutokea kwa tukio hili na kuahidi kulizungumzia kesho Jumapili Julai 14, 2019.