Halmashauri 31 zamkera Waziri Jafo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo

Muktasari:

 

  • Halmashauri 31 ambazo zimeshindwa kutoa fedha za lishe zatakiwa kujieleza sababu za kushindwa kufanya hivyo.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ameagiza halmashauri 31 ambazo zimeshindwa kutoa fedha za lishe kujieleza kwa wakuu wa mikoa ndani ya siku 14 sababu ya kushindwa kwao.

Aidha Jafo amesema sika sababu za kushindwa kwao na taarifa iwasilishwe Tamisemi baada ya siku 21.

Jafo amesema hayo jijini Dodoma jana Jumanne Machi 19 mwaka 2019 wakati akizungumzia namna huduma za lishe zinavyoendelea nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri na wadau wa lishe.

“Tatizo ni utoaji wa fedha zilizotengwa kwenye lishe. Eneo ambalo halifanyi vizuri tusitarajie kupata matokeo mazuri.”

“Kuna halmashauri 31 wameshindwa kufanya hivyo, bado kuna halmashauri 21 zimeshindwa kutimiza mikataba ambayo mlikubaliana,” amesema.

Jafo amesema Desemba 19 mwaka 2017 alisainishana mikataba na wakuu wa mikoa kuhusu usimamizi wa masuala ya lishe.

“Kuna mikoa inafanya vizuri mingine inasuasua, kuna halmashauri zinafanya vizuri lakini zingine zinasuasua,” amesema.

Amesema inawezekana watu wanaona suala la lishe ni la mzaa sana wakati linatakiwa kuchukuliwa hatua huku akidai kuwa kwenye mikoa 10 pekee kuna watoto 1,000 wenye tatizo la vichwa vikubwa.

“Kwenye udumavu rasilimali akili zinapungua. Watoto wenye udumavu darasani hawaelewi. Hili eneo linaweza kuwa kikwazo kwetu kwenye kufikia uchumi wa kati kama tusipotilia mkazo,” amesema

Amesema hali ya usimamizi wa masuala ya lishe imeimarika tofauti na awali na kuwataka wakuu hao kutilia mkazo.

“Kuna mikoa ilifanya vizuri lakini tathmini ya sasa baadhi ya mikoa imerudi nyuma hili si jambo jema kwenye usimamizi wa lishe,” amesema.

Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Joseph Nyamhanga amesema katika

bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa 2019/20 zimetengwa Sh50 bilioni kwa ajili

ya lishe.