Halmashauri zashindwa kufikia lengo makusanyo

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa Seleman Jafo akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri Mwita Waitara na Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo Tixson Nzunda

Muktasari:

  • Waziri wa nchi ofisini ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo leo amezungumzia ukusanyaji wa mapato katika nusu ya mwaka wa fedha 2018/19 huku Dodoma ikiongoza na Tanga ikishika mkia.

Dodoma. Waziri wa nchi ofisini ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amesema halmashauri zilipanga kukusanya Sh 735.6 bilioni lakini hadi mwishoni mwa Desemba 2018 makusanyo yalikuwa Sh300 bilioni ambayo ni asilimia 41.

Amesema jiji la Dodoma limeongoza tena kwa mapato katika nusu ya mwaka wa fedha 2018/19.

Dodoma imeongoza kwa kukusanya Sh40.12 bilioni ikiwa ni asilimia 59 ya mapato yake huku ikishika nafasi ya pili kwa jumla baada ya kukusanya Sh 44.8 bilioni nyuma ya Dar es Salaam iliyokusanya Sh 77.04 bilioni.

Jafo amewaeleza hayo waandishi wa habari leo jijini Dodoma wakati akizungumzia makusanyo ya Serikali.

Alisema halmashauri zilipanga kukusanya Sh 735.6 bilioni lakini hadi mwishoni mwa Desemba 2018 makusanyo yalikuwa Sh300 bilioni ambayo ni asilimia 41.

Wakati Dodoma ikiongoza kwa majiji,  Tanga imekuwa ya mwisho wakati huo baada ya kukusanya kwa asilimia 33 na wilaya ya Nanyumbu ni ya mwisho kwa makusanyo katika mpangilio wa jumla ikikusanya kwa asilimia 6.