Hapi: Watendaji wasioweza kazi watafute mkoa wa kuhamia

Friday March 22 2019Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi 

By Berdina Majinge, Mwananchi [email protected] co.tz

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewataka watendaji wa Serikali ya mkoa huo kujitathimini kwa kutatua migogoro na kero za wananchi na endapo mtendaji ataona hatoshi hana budi kuhama mkoa.

Hapi amesema hayo leo Machi 22, 2019 katika ofisi ya kata Kitanzini wakati akiendelea na ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa huo. Amesema watendaji hao hawana budi kubadilika au kutafuta kazi mikoa mingine.

Hapi amesema ziara yake ya ‘Tunakufuata ulipo’ ina lengo la kutatua kero za wananchi, kuwatumikia wananchi na kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi.

"Serikali ina jukumu la kuwasikiliza wananchi, migogoro ya ardhi imekuwa ni jambo linalowanyima usingizi wananchi walio wengi, kuna wajane wananyanyasika, wapo waliopoteza maisha kwa ajili ya migogoro ya ardhi," amesema.

Hapi amesema manispaa ya Iringa ndio inaongoza kwa migogoro ya ardhi na wataalam ndio wanaoongoza kwa kutengeneza migogoro na kusababisha wananchi wanyonge kukosa haki.

"Sitamvumilia mtendaji yeyote wa Serikali au mtaalam aliyegeuka kiwanda cha kutengeneza migogoro kwa kupindua sheria na taratibu na kuzikanyaga na kusababisha wanyonge kunyanyasika na kukosa haki, wachague kubadilika ama kuhama mkoa," amesema Hapi.

Advertisement

Amesema watu wanyonge kupata haki ni sawa na urefu wa mbingu na ardhi, ukiwa na fedha kidogo watumishi watakuheshimu, hivyo amewataka watumishi kuacha kutengeneza migogoro ili kujipatia fedha na kuwanyima haki wanyonge.

"Mimi siwezi kukaa ofisini wakati wananchi wanyonge wanateseka, ni unyanyasaji kumzuia mwananchi kukarabati nyumba na kumtaka ajenge ghorofa ilihali ni raia ambao hawana uwezo wa kujenga ghorofa, nimebaini mpango huu ulikuwa ni hamisha maskini mjini," amesema.

“Waacheni watu maskini wabomoe na kukarabati nyumba zao na hakuna mtu atakayebadilisha uamuzi huo sitaki kusikia wananchi amehamishwa au kuzuiwa kukarabati nyumba, nawahakikishia sauti ya wengi ni sauti ya Mungu," amesema.

Advertisement