Harden aifungia rockets pointi 50 kwa mara ya saba ligi ya NBA

Muktasari:

Nyota huyo wa Houston Rockets aliiongoza timu yake kushinda dhidi ya Miami Heat katika mchezo wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani iliyochezwa kwenye uwanja wa Toyota Center jana.

 


James Harden jana alifunga zaidi ya pointi 50 kwa mara ya saba na kutoa pasi 10 kwa wafungaji wakati alipoiongoza Houston Rockets kuishinda Miami Heat kwa pointi 121-118 katika mechi ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani.

Katika kipindi cha mechi chache ambacho Harden alikuwa akichemsha kufunga kwa three-pointer, Rockets ilikuwa ikitegemea akiba yake kufanikisha kazi.

Lakini Harden alijifufua juzi mbele ya mashabiki wa nyumbani wapatao 18,100 walioojazana uwanja wa Toyota Center na kumaliza mchezo huo akiwa amefunga pointi 58 na kutoa assisti 10, huku akiokoa mipira mara saba katika usiku ambao Rockets ilijikuta ikifanya kazi kubwa ya kuibuka na ushindi licha ya kusumbuliwa namajeruhi.

"Nilitaka kuwa na ujasiri na kuendelea kufunga," alisema Harden. "Nilirusha mipira kufunga pale nilipopata nafasi."

Alipata msaada kutoka kwa Austin Rivers aliyefunga pointi 17 na Chris Paul, ambaye pointi alizofunga sekunde 46 kabla ya mchezo kuisha baada ya jaribio la Harden la kufunga three-pointer kufeli, ziliifanya Rockets kuongoza kwa pointi tatu zaidi.

Harden ameshafunga pointi 50 na kutoa assisti 10 mara tatu msimu huu. Wimbi lake la kufunga pointi 30 mfululizo lilizuiwa katika mechi ya 32 Jumatatu dhidi Atlanta Hawks.

"Tuliangalia karatasi ya matokeo baada ya mechi, niliona amefunga pointi 58," alisema mchezaji mwenzake, Rivers. "Wote tulikuwa kama tunasema 'alifunga pointi zote hizo. Ni nyingi sana. Huwezi kuamini."

Mwezi uliopita Harden alifunga pointi 61, ambazo ni kiwango cha juu kwake tangu aanze kucheza NBA alipoiongoza Rockets kushinda kwa pointi 114-110 dhidi ya New York Knicks.

Katika dakika za mwisho, Miami iliongoza kwa pointi 113-103 baada ya Goran Dragic kufunga kwa three-pointer zikiwa zimesalia dakika 6:18, lakini Houston ikazinduka na kufunga pointi 14 bila ya majibu na kurejesha uongozi. AFP