Hata kidogo ulichonacho kinaweza kukufanikisha, using’ang’ane na kikubwa

Nabii James Nyakia

Muktasari:

Shaloom, Shaloom wana wa Mungu, Jina langu naitwa Nabii James Nyakia kutoka Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda jijini Dar es Salaam.

Leo Mungu amenipatia kibali cha kuzungumza nawe kuhusu jambo muhimu linaloitwa ‘kushinda kabla ya kushinda’.

Unapofanya jambo lolote katika maisha yako unatarajia matokeo fulani na zaidi ni ushindi. Hivyo lazima uwe na malengo kabla ya kukifanya kitu hicho.

Mungu amenipa neema ya kuzungumza nawe kwamba kila kitu unachofanya ona kuwa umeshinda kabla hata ya kuanza kukifanya.

Kuna aina mbili za kuona kitu. Kingine unaweza kukiona kwa macho lakini kipo ambacho hakionekani.

Kisichoonekana kwa macho lakini kipo kwenye akili kinaitwa maono na kile unachokiona kwa macho ni kitu ambacho tayari kimeumbwa.

Kwa hiyo unapofanya kitu au jambo la aina yoyote ile kwa maono unafanya kwa nguvu ya Mungu.

Ili uweze kushinda kabla ya kushinda lazima utumie kitu ulichonacho kwa usahihi.

Usitamani kupata kitu ambacho kipo juu ya uwezo wako au kitu cha mtu mwingine kwa kudhani unaweza kushinda kwa kutumia hicho.

Kitu kidogo ulichonacho ni cha thamani lakini ili ufanikiwe lazima utumie maarifa, ujitambue, uwe mvumilivu na uambatane na watu sahihi.

Wafalme 2;7 neno la Mungu linasema ‘Basi watu 50 wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama kuwakabili kwa mbali, hao wawili wakasimama karibu na Yordan, Eliya akalitwaa vazi lake la juu akalikunja, akapiga maji, yakagawanyika huku na huko na hao wawili wakavuka pakavu’.

Wakati Eliya anavuka hakuwa na kitu chochote kile isipokuwa vazi la nguo yake tu.

Unaweza kujiuliza ni kitu gani cha kwanza ambacho Mungu amekupa?

Unadhani unashindwa kufanya vitu vikubwa kwa sababu hauna elimu? Au umezaliwa katika familia masikini sana au wewe ni yatima kwamba wazazi wangekuwepo wangekusaidia?

Unafikiri kwa sababu umekulia kijijini ndio maana huwezi kufanya jambo lolote.

Hapana. Tumia hicho kidogo ulichonacho kufanya kama mtaji wa kukufikisha kwenye kikubwa usichonacho.

Kwa hicho kidogo ukipiga magoti na kumuomba Mungu ukimwambia hiki ndicho nahitaji kinipatie hatua kubwa zaidi, Mungu atasimama kwa ajili yako na utafanikiwa.

Siku moja mama mmoja alikuja kuomba msaada kwa sababu ni mjane.

Nilimuuliza mama unafanya nini? Aliniambia ‘maisha ni magumu sana, ndugu wa mume wangu wameninyang’anya kila kitu’.

Nikauliza sasa unaishije na watoto, akasema ‘nabii sina namna ya kuishi hivi unavyoniona sina chochote kila siku napita naomba’.

Nikamwambia hebu chukua hii Sh20,000 kwa neema ya Mungu nikamwambia, using’ang’ane uwe na mtaji mkubwa sana ndipo ufanikiwe.

Pesa hii nenda kauze njugu mawe. Hakikisha njugu mawe zako unaandaa katika mazingira mazuri, unga vizuri uwe mtamu na hakikisha unaanza kuuza mapema wakati watu wanahitaji kunywa.

Nilimwambia usiogope, kapige debe ukitangaza biashara yako.

Mama alifanya kama nilivyomuelekeza na leo hii faida yake kwa siku inafikia Sh80,000.

Mungu anahitaji uwe na maamuzi sahihi na uambatane na watu sahihi. Unaweza kuwa unaumia kwamba labda sababu ni kuwa huna elimu.

Hebu fikiria, ni watu wangapi waliosoma lakini wanahangaika hawana kazi, wanaishi kwenye nyumba za kupanga, wana madeni kiasi cha nyumba zao kuuzwa kwa mnada.

Ukiona unaishi ujue kwamba unaishi kwa sababu Mungu anayo makusudi katika maisha yako.

Using’ang’ane kupata kile ambacho kipo mbele yako na huna uwezo wa kupata kwa wakati huu, ng’ang’ana na kile ulicho na uwezo nacho.

Ukitaka kufanikiwa katika malengo yako usitake ufanane na mtu fulani.

Jiulize tu maswali machache, hivi naishi ili iweje? Jua lengo la kuishi kwako.

Kuna mtu tunavyoongea yupo hoi kitandani, anachoomba ni neema tu ya kupona. Mwingine amekufa hatambui hata kama alikuwa anamiliki magari.

Upo hai, Mungu amekupa neema ya kupumua jiulize kwanini upo mahali ulipo? Ni sehemu sahihi? Kina nani wanakuzunguka?

Kumbuka duniani tunakutana na watu wa aina mbili tu, wema na wabaya. Je hao ulio nao ni watu wa aina gani? Ni sahihi kwako? Wanaweza kuwa daraja kwenye maisha yako?

Kwa hiyo kila unayekutana naye uwe makini. Jiulize kwa nini mpaka sasa kuna watu nilikua nao hawapo duniani, jibu lake moja tu, ni kwa sababu Mungu anamalengo nawe ndio maana upo hai.

Jambo jingine jifunze kuthamini kitu chochote kile unachopata.

Elimu yako umeitumia kufanya jambo gani? Inaweza kuwa huna elimu ya darasani ila umepata elimu ya duniani kutoka kwa wazazi wako.