Hatima Maalim Seif yabaki mahakamani

Katibu Mkuu mpya wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa (kushoto) akipongezana na Naibu Katibu mkuu Zanziba, Fakhi Suleiman Khatibu baada ya kutangazwa kushika nyazifa hizo jana.Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Hatima ya Maalim Seif Shariff Hamad kuendelea kuwa katibu mkuu wa CUF, hivi sasa imebakia mikononi mwa Mahakama.

Hatua hiyo inafuatia CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba kumtangaza Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu mpya wa chama hicho jana, baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi.

Mbali na Khalifa, wengine walioteuliwa ni manaibu katibu mkuu (Bara), Magdalena Sakaya na Fakhi Suleiman Khatibu (Zanzibar).

Hata hivyo, hatima ya viongozi hao wapya wa CUF akiwamo Profesa Lipumba aliyechaguliwa na mkutano mkuu Jumatano wiki hii kuwa mwenyekiti itajulikana baada ya hukumu itakayotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu kesho.

Hukumu hiyo ni ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachana wanaomuunga mkono Maalim Seif, wakipinga uhalali wa Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti. Wanachama hao wanampinga Profesa Lipumba ambaye Agosti 2015 alitangaza kujizulu nafasi hiyo kisha baadaye akatangaza kurejea, hali iliyoibua mgogoro wa kiuongozi.

Mgogoro huo umekigawa chama hicho katika pande mbili - ule wa Profesa Lipumba na wa Maalim Seif, hivyo hukumu hiyo ambayo inasubiriwa na wanachama wengi itaamua hatima ya pande hizo.

Mara baada ya Khalifa kutangazwa makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam jana alisema jambo la msingi ni kuimarisha umoja na kuaminiana.

Akizungumza baada ya kutangazwa, Khalifa aliyewahi kuwa mbunge Gando alisema upande wa Zanzibar watu wamedanganywa kuwa kila kinachosemwa na upande wa Maalim Seif ni kweli, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya siasa.

Alisema iwapo kuna mtu alikuwa anajua kuwa ana nafasi ndani ya chama, ajiandae kukubaliana na mazingira mapya kwa sababu mkutano mkuu umefanya uchaguzi uliosimamiwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na viongozi wamepatikana.

“Haya yote ni mabadiliko ambayo yamefanywa, aliyekuwa na nafasi fulani sasa ajipange kukubaliana na hali iliyopo, akijidai hayatambui (mabadiliko) anajidanganya kwa sababu yamehudhuriwa na msajili wa vyama vya siasa na ameuridhia mkutano mkuu, kama yupo aliyenuna sana anaweza akakaa kimya,” alisema Khalifa.

Alisema jambo la kwanza atakalolifanya ni kufufua umoja wa kitaifa, kuhamasisha wanachama kusahau chuki na fitina zilizokuwapo kabla ya uchaguzi na kuhubiri siasa za kidemokrasia.

Alisema jambo ambalo hatalisahau katika mgogoro baina ya pande hizo mbili ni namna alivyokuwa anatatizika. “Ilikuwa inaniathiri kisaikolojia kwa sababu ukweli upo wazi na unajulikana, lakini unapindishwa na kupandikizwa uongo ambao hata aliyeuongopa anauamini.”

Naibu Katibu Mkuu (Bara), Sakaya alisema watashirikiana na vyama vya siasa iwapo vitakuwa na nia ya kuleta mabadiliko ya kweli na si kuvitumia vyama vingine.

“Siasa siyo vita wala chuki, kilichotokea kwenye mkutano mkuu siyo siri kila mmoja amekiona, hivyo tunachokwenda kufanya ni kushirikiana kuhakikisha demokrasia ya nchi hii inapatikana na wananchi wanapata maendeleo,” alisema Sakaya ambaye ni mbunge wa Kaliua.

Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Fakhi alisema anamheshimu Maalim Seif na akikutana naye atamweleza kilichojiri kwenye mkutano mkuu ikiwamo kupatikana kwa mwenyekiti na katibu mkuu wa chama hicho kwa njia ya amani.