Hatimaye Madonna kutumbuiza Israel Jumamosi

Thursday May 16 2019

 

Jerusalem, Israel/AFP. Madonna amesaini mkataba wa kutumbuiza katika shindano la muziki la Eurovision nchini Israel na kumaliza hali ya utata iliyokuwepo baada ya wito wa kumtaka agomee kushiriki, shirika la utangazaji la Serikali, KAN limesema leo Alhamisi.

"Sasa ni rasmi," KAN, ambayo inatayarisha shindano hilo kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Ulaya (EBU) iliandika katika tovuti yake.

"Baada ya siku za hali tete, mkataba kati ya Madonna na watayarishaji wa Eurovision umesainiwa leo," KAN ilisema.

Nyota huyo wa muziki wa pop mwenye umri wa miaka 60 alisema Jumanne kuwa amepania kutumbuiza katika fainali hizo za mashindano ya kuimba zitakazofanyika Tel Aviv Jumamosi.

Lakini EBU ilisema siku moja kabla kabla ya tamko hilo kuwa mkataba wa mwisho wa ushiriki wake ulikuwa haujakamilishwa.

Hadi Alhamisi vyombo vya habari vya Israel vilikuwa vikiripoti kuwa kulikuwa hakuna mkataba na EBU na KAN walikuwa wakikataa kutoa taarifa za maendeleo ya suala hilo.

Watayarishaji wa Madonna walisema mwezsi Aprili kuwa nyota huyo atatumbuiza katika shindano hilo katika mji wa Tel Aviv, ambao uliteuliwa kuwa mwenyeji wa fainali baada ya mwimbaji wa Israeli, Netta Barzilai kushinda nchini Ureno mwaka jana.

Lakini ushiriki wake uliibua pingamizi kutoka wanaharakati wa Divestment and Sanctions (BDS), ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikipiga kampeni kutaka wawekezaji na wasanii wasishirikiane na Israel kutokana na nchi hiyo kukalia ardhi ya Palestina kwa miaka mingi sasa.

"Sitaacha kufanya muziki kwa ajili ya kufurahisha ajenda ya kisiasa ya mtu fulani na wala sitaacha kwa ajili ya kuzungumza dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoweza kuwa unafanyika popote pale duniani," alisema Madonna katika taarifa iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Marekani Jumanne.

Madonna ataenda na kundi la watu 135, akiwemo rapa KoVu, na waimbaji waitikiaji 40, madansa 25 na timu ya mafundi, kwa mujibu wa ripoti inayomtaja bilionea wa Canada mwenye asili ya Israel, Sylvan Adams, kuwa ndiye anayegharimia onyesho lake.

Washiriki 26 kati ya 41 watachuana kuwania nafasi ya kwanza ya shindano hilo litakalorushwa kwa saa tatu na nusu Jumamosi.

Madonna atatumbuiza wakati wa mapumziko.


Advertisement