Hatua kwa hatua sakata la korosho

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (kulia) akiangalia shehena ya magunia yenye korosho alipokwenda kukaguwa maghala yanayohifadhi korosho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga alipofanya ziara ya kikazi mkoani Pwani. Picha na Mathias Canal

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa ununuzi huo wa korosho, Mwananchi limechambua matukio mbalimbali yaliyotokea tangu mwaka jana sakata hilo lilipoibuka bungeni.

Dar es Salaam. Zao la korosho limeibua mjadala tangu mwaka jana baada ya bei kupanda hadi Sh4,000 kwa kilo na baadaye kusababisha mzozo bungeni wakati Serikali ilipowasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria kuhusu mgawanyo wa fedha za ushuru kabla ya bei kushuka msimu huu.

Mzozo huo wa bei ulisababisha Rais John Magufuli kuingilia kati na kutaka kilo moja inunuliwe kwa Sh3,300 tofauti na bei waliyotaka wafanyabiashara ambayo ni chini ya Sh3,000.

Korosho ni zao linaloongoza kwa kuchangia Pato la Taifa na kwa mujibu Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) katika msimu wa 2017/2018 mapato ya zao hilo yalifikia Sh1.08 trilioni, ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.

Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa ununuzi huo wa korosho, Mwananchi limechambua matukio mbalimbali yaliyotokea tangu mwaka jana sakata hilo lilipoibuka bungeni.

Yaliyotokea

Mei 24, 2018: Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alitoa hoja bungeni akilitaka Bunge lijadili suala la ‘export levy’ (tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi) ambalo aliliita la dharura akisema Serikali kuendelea kukamata fedha hizo ni hujuma.

Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe walimuunga mkono kabla ya kiongozi huyo wa chombo cha kutunga sheria kusema Wizara ya Fedha inapaswa kujitathimini kwa kuwa fedha hizo inabidi zirudishwe kwa wakulima kwa mujibu wa sheria.

Juni 20, 2018: Mbunge wa Kilwa (CUF), Suleiman Bungura alitishia kuwa wakulima na wabunge wa mikoa ya kusini wangeandamana endapo Serikali haitawapa wakulima asilimia 65 ya ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi.

Juni 22, 2018: Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Abdallah Bulembo aliiangukia Serikali akiitaka ipeleke fedha za wakulima wa korosho kwa maelezo kuwa isipofanya hivyo itawagharimu katika chaguzi zijazo.

“Pelekeni haraka fedha za korosho jamani. Mnapotaka kuua zao la korosho, pamba na kahawa kwa wakulima mnawaza nini? Hivi hiyo hela ni yetu kweli? Hiki ni chao wapeni,” alisema Bulembo.

Kutotolewa kwa fedha hizo ambazo zilikuwa zinatumika kuweka urahisi wa bei ya pembejeo za korosho kulisababisha salfa kupanda bei kutoka Sh16,000 hadi 70,000 jambo ambalo lilitajwa kuwa lingeathiri mavuno ya msimu ujao.

Oktoba 22, 2018: Mnada wa kwanza wa korosho ulipofanyika, wakulima waligoma kuuza korosho zao kwa bei ya kati ya Sh1,711 na 2,712 wakidai kuwa gharama hiyo ni ndogo ikilinganishwa na gharama za uzalishaji.

Oktoba 26, 2018: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya kikao cha wakuu wa mikoa inayolima korosho, alimfuta kazi Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho na kumwagiza Waziri wa Kilimo kumrejesha wizarani.

Siku hiyohiyo alisimamisha minada ya zao hilo kwa siku tano hadi Novemba Mosi.

Oktoba 28, 2018: Baada ya wakulima kugoma kuuza korosho katika minada minne mfululizo kwa kile walichoeleza kuwa ni bei ndogo, Rais John Magufuli alifanya mkutano na wadau wa korosho na kuwataka wafanyabiashara kununua korosho hiyo kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

Novemba 2, 2018: Mnada wa kwanza ulifanyika baada ya agizo la Rais. Wafanyabiashara kadhaa walijitokeza, jumla ya tani zilizonunuliwa katika minada miwili zilikuwa tani 2,341 na bei ya juu ilikuwa Sh3,016 kwa kilo moja, lakini wengi waliishia Sh3,000.

Novemba 9, 2018: Rais Magufuli alifanya ukaguzi wa magari ya jeshi yatakayosomba korosho endapo wafanyabiashara hawatafanya hivyo hadi kufikia Novemba 12.

Novemba 10, 2018: Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Anna Abdallah na kuivunja bodi hiyo kuanzia siku hiyo.

Novemba 12, 2018: Rais alitangaza kuwa Serikali itanunua korosho zote na hakuna haja ya kuwauzia wafanyabiashara kwakuwa wataleta matatizo huku wakulima wakihangaika.

Novemba 24, 2018: Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara alisema Serikali itahakikisha korosho zote zinazonunuliwa kwa wakulima zinabanguliwa nchini.

Desemba 29, 2018: Serikali ilizifunga kwa muda akaunti 191 za benki zinazomilikiwa na wakulima wa korosho kupisha uhakiki wa kina wa umiliki wa korosho walizouza ikiwa tayari imewaingizia Sh3.8 bilioni.

Januari 27, 2019: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliiagiza Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kuhakikisha wanakamilisha uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho hadi Februari 5.

Januari 30, 2019: Serikali iliingia makubaliano na kampuni ya Indo Power Solutions ya nchini Kenya juu ya ununuzi wa tani 100,000.

Februari 5, 2019: Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilitaja mambo saba katika kukabiliana na changamoto ya zao la korosho ikiwamo uhakiki wa uwazi unaowashirikisha wakulima wenyewe au vyama vyao vya ushirika na masoko.

Februari 7, 2019: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa ufafanuzi kwanini kuna wakulima wanalipwa Sh2,600 badala ya Sh3,300 akisema bei ya Sh3,300 ni kwa ajili ya korosho daraja la kwanza tu.

Februari 20, 2019: Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda aliwakaribisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kununua korosho ghafi kiasi cha tani 221,060.