Hawa ndio maadui wa demokrasia yetu

Wanataaluma wa fani ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma wametofautisha hadhira ya vyombo vya habari kwa kuigawanya katika makundi matatu. Mimi nitaongeza moja la nne. Makundi haya manne yana uhusiano mkubwa na maendeleo ya kisiasa, hususan siasa za kidemokrasia.

Makundi haya yametajwa na Davis “Buzz” Merritt, Maxwell E. McCombs katika kitabu chao kiitwacho: ‘The Two W’s of Journalism: The Why and What of Public Affairs Reporting.’

Kundi la kwanza linaitwa, wasaka taarifa. Hawa ni wafuatiliaji makini wa mambo, wakitaka kujua karibu kila jambo linalohusiana na ustawi wa jamii iwe katika siasa, uchumi, jamii na kadhalika. Aina hii ya watu wana hamu ya kutaka kujua mambo, wana uelewa mkubwa na ni wadadisi wanaotafuta taarifa za kina kuhusu jambo fulani.

Watu wa kundi hili ni hadhira nzuri ya vyombo vya habari, kila siku wananunua magazeti makuu (siyo ya udaku) au wakipita popote yanapopatikana magazeti, mathalan maktaba, hupoteza muda mrefu kujisomea. Saa mbili usiku, utawakuta wanaangalia habari katika runinga bila kukosa. Wengine utawakuta katika mitandao ya habari inayojadili habari ngumu zinazoigusa jamii kama Twitter, wakifuatilia au mara nyingine kujadili mambo.

Wazee wa kuperuzi

Kundi la pili ni lile la watu wa kati. ‘Watu wa kuperuzi’ wanaopitia habari kijuujuu. Hata hivyo, kundi hili la watu, wakiperuzi na kukutana na habari yenye kuwagusa moja kwa moja hulitafutia undani wake. Aina hii ya watu utawaona wanapoingia mahali penye magazeti, ataangalia kurasa za mbele na nyuma, kisha huyoo aenda zake.

Mtu wa kundi hili atawahi mapema kuangalia vichwa vya habari katika taarifa za habari za runinga, na akiona hakuna linalomgusa moja kwa moja atahamia kwenye mambo mengine. Likiwapo linalomuhusu na kumuathiri, ataendelea kuangalia mpaka alijue hilo kwanza.

Watu wa nyepesi nyepesi

Hawa, ukiwakuta wanaangalia runinga, itakuwa tamthilia, filamu au muziki na mambo mengine kama hayo ambayo hayahusiani na mambo muhimu ya kiraia na kijamii. Magazeti yao ni ya michezo na udaku, akisoma gazeti makini ataanzia ukurasa wa nyuma kwenda mbele. Vituo vya redio vyao ni hivi vya kisasa vya vijana wakisikiliza taarabu, bongo fleva, singeli na kadhalika.

Watu wa aina hii kutwa utawakuta Instagram wakifuatilia maisha ya watu maarufu huku wakijinasibisha na timu za watu hao. Utasikia: “Mimi timu Wema,” mwingine Zari, mwingine Hamisa na kadhalika. Utaona wanalalamika mitandaoni kwa nini Jux na Vanessa wameachana. Maishakwa kwao ni burudani tu.

Kundi la nne

Kundi la nne ni la hatari sana. Hawa hawana muda wa kufuatilia habari kabisa. Kwa sababu hawana muda wa kufuatilia mambo muhimu ya umma, hawashughulishwi na chochote katika masuala ya kiraia, si ya siasa, si ya uchumi wala si ya kijamii. Ni kama wapo kisiwani au katika dunia yao isiyoingiliana na maisha ya wanajamii wenzao.

Hili kwa kiasi fulani linafanana na lile la tatu kwa sababu wote hawajishughulishi na mambo muhimu ya kiraia. Lakini, wana tofauti moja, la tatu walau wanatumia vyombo vya habari kuliko la nne.

Maadui wa demokrasia

Ubora wa raia katika nchi unapimika kwa ufuatiliaji na ufahamu wao wa mambo ya kiraia yaani kutafuta taarifa muhimu za mambo ya umma na kuzifanyia kazi.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya ubora wa raia katika nchi na hali ya demokrasia katika nchi husika.

Kwa msingi huo ndio unaweza kuona umuhimu wa kuyafahamu makundi manne niliyoyataja hapo juu – kundi lipi linafaa na lipi halifai, na nini kifanyike kuwahamisha kutoka kundi lisilofaa kwenda wanapotakiwa ili demokrasia ifanye kazi na tuone matunda yake.

Makundi yote hayo yapo katika jamii yoyote, kwa asilimia tofauti. Katika ulimwengu wa Magharibi, waliamini kundi linalotawala ni lile la kwanza la watu makini, wasaka taarifa. Hata hivyo, kupitia ushahidi mbalimbali inaonekana kuwa kundi la pili, wale wazee wa kuperuzi, ndio hasa walio wengi. Hawa, hujali yanayowahusu na yasiyowahusu huyapotezea.

Hali ya Tanzania

Kwa hapa sina majibu yanayotokana na utafiti, lakini naweza kukupa viashiria. Vipo vya kitabia na vya matokeo.

Viashiria vya kitabia ni vile tunavyoviona katika mienendo ya watu katika utumiaji wa vyombo vya habari. Mfano, usomaji wa magazeti? Gazeti gani kubwa linalochapisha nakala nyingi zaidi, labda elfu 40? Nasikia ukijumlisha mauzo ya magazeti yote ya kila siku (si udaku na michezo), wanauza nakala zisizozidi elfu 80. Linganisha idadi hiyo na wakazi milioni 4.5 wa Dar es Salaam (sensa ya 2002), kati yao labda milioni 1.5 ndio watu wazima. Linganisha na kaya zaidi ya milioni moja za jiji hili, pia kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.

Pale chuo kikuu, Shule Kuu ya Waandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), wanafunzi wangu huenda kusoma magazeti maktaba pale tu wanapopewa kazi za darasani zinazowataka kufanya hivyo. Vinginevyo, wao Instagram, wakitembelea kurasa za mastaa na umbeya. Hawa wanaakisi vijana wengi wa sasa. Wachache mno pia huangalia taarifa za habari za runinga.

Viashiria vya matokeo

Aina hiyo ya Watanzania wasiojali, ndio ambao hata litokee jambo kubwa linaloathiri watu, wao ni ‘hewala’. Hawaoni kabisa uhusiano wa majanga yanayowakabili - ukosefu wa ajira, mitaro michafu mbele ya nyumba zao, huduma mbaya na ghali hospitalini na uongozi wa kisiasa katika nchi yao.

Nikupe mfano. Mbele ya nyumba ninayoishi kumepita mfereji wa maji machafu ambao umetengenezwa kama sehemu ya miundombinu ya barabara kwa ajili ya kupeleka maji machafu yanapotakiwa kwenda. Hali ya usafi katika mfereji ule ni mbaya mno. Takataka nyingi zimeingia na kuzalisha uozo wa kutisha.

Wakati mfereji ule ukitoa uvundo, serikali ya mtaa inapita kila siku kukusanya fedha za kubeba takataka. Juzijuzi wakatwambia tusafishe sehemu ya mfereji iliyo mbele ya eneo la nyumba.

Tukafanya hivyo, tukaweka takataka barabarani. Gari la takataka lilipofika lilisomba za kutoka majumbani na kuacha zile za mferejini. Hakuna aliyeuliza. Hakuna aliyejali.

Kila nipitapo nasikia malalamiko ya gharama kubwa za matibabu zisizohimilika kwa watu masikini katika hospitali kubwa hapa nchini, hususan Hospitali ya Taifa Muhimbili. Ndugu wa jamaa yangu mmoja, sasa marehemu, nikasikia katoroka matibabu baada ya kugundua asingeweza kumudu gharama.

Malalamiko ni mengi lakini kwa sababu ya idadi kubwa ya wananchi wetu ni lile kundi la tatu na la nne, yaani wanaotumia vyombo vya habari kwa kujipumbaza na wale wasiotumia kabisa; inashindikana kung’amua uhusiano wa matatizo yanayotuzunguka na hali ya uongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali. Wale wa kundi la tatu na nne ndio maadui wa kweli wa demokrasia, sio viongozi wa Serikali na chama. Kufanikiwa kwao kunategemeana na nchi husika, ina watu wanaojali au wasiojali?