Heche adai Serikali ya Tanzania imeshindwa kutekeleza mambo matatu

Mbunge wa Tarime Mjini, John Heche akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ameeleza mambo matatu akidai hayajatekelezwa na Serikali licha ya kuahidi kabla ya kuingia madarakani, kusisitiza kwa kitendo hicho kinaifanya kukosa uhalali wa kuendelea kubaki madarakani.


Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeshindwa kutekeleza ahadi nyingi ilizoahidi mwaka 2015 na haoni kama itafanya hivyo kwa sababu umebaki mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Heche alitoa kauli hiyo jana jioni Jumatano Juni 19, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

“Hii ni bajeti yenu ya nne na ya mwisho kwa kuwa naamini inayokuja itatekelezwa na Serikali nyingine maana hamtakuwa madarakani, mlitoa ahadi za uongo kuwa kila kijiji mtapeleka Sh50milioni, hivi fedha ziko wapi? Hili haliwezi kupita hivihivi,” alisema Heche.

Alisema Serikali ya Tanzania iliahidi kutoa pensheni kwa wazee jambo alilodai hadi sasa kuwa halijafanyika.

“Katika ilani yenu (Ilani ya uchaguzi wa CCM) mliandika, sasa ndio mseme mliandika uongo na kuwapotosha Watanzania hampaswi kuchaguliwa hata kijiji kimoja,” alisema mbunge huyo.

Pia, aligusia suala la nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma, “Nataka nikupe data kidogo mwaka 2010 mpaka 2014 katika uongozi wa Rais Jakaya Kikwete watumishi wa kada ya afya walioajiriwa walikuwa 42,800, ila nyinyi mwaka 2015 hadi sasa mmeajiri  watumishi wa kada ya afya 10,000 peke yake.”

Alisema kuna vijana 75,000 waliomaliza vyuo vya ualimu nchini, wapo mtaani wakisaka ajira

“Mtawaajiri lini watoke nyumbani, je mnatakiwa kuchaguliwa kweli? Msiwambie watu wale mtori nyama iko chini, wanataka kula nyama kama nyie. Wambieni mnatoa lini ajira,” alisema Heche.

Mbunge huyo pia aligusia mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji, kuitaka Serikali ieleze megawati ngapi zitaanza kuzalishwa, na hatua ngapi zitapita ili mradi huo uanze kuzalisha megawati 2,115 na itakuwa lini.