Heche ahoji kwa nini Serikali ya Tanzania imeshindwa na Gazeti la Kenya

Mbunge wa Tarime Vijini (Chadema), John Heche

Muktasari:

Mbunge wa Tarime Vijini (Chadema), John Heche amechangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2019/20 akisema Serikali isiendelee kuikingia kifua Kampuni ya Indo Power Solution ya Kenya iliyokuwa inunue korosho za Tanzania

Dodoma. Mbunge wa Tarime Vijini (Chadema), John Heche amesema Serikali haipaswa na haitafanikiwa kuikingia kifua kampuni ya Indo Power Solution ya Kenya iliyoingia mkataba wa ununuzi wa korosho na Serikali ya Tanzania.

Amesema ni aibu kwa Serikali kushindwa kubaini kampuni hiyo ni hewa na jukumu hilo likafanywa na mwandishi mmoja pekee wa Gazeti la Daily Nation la Kenya ambalo lilibaini kampuni hiyo haipo nchini humo na wala haina ofisi.

Heche amesema hayo leo Ijumaa Mei 17, 2019 bungeni wakati akichangia bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2019/20 ya Sh253.85 bilioni.

Ameanza kuchangia akisema kati ya mambo ambayo Serikali imefanikiwa kuyafanya yadharaulike ni kilimo na ualimu.

“Mtu akitaka kufeli utasikia mtu anasema umeshindwa hata ualimu au utasikia utarudi kulima.

 

“Tangu mmeingia madarakani miaka mitatu, bei ya Kahawa ilikuwa Sh2,200 pale Tarime lakini sasa imefikia Sh800, tunakwenda mbele au tunarudi nyuma,” amehoji.

 

Amesema mawaziri wanalipwa fedha za walipa kodi, mnafungiwa mikanda katika magari, mafuta ya magari yenu mnalipwa kwa kodi za wananchi, “tunaposimama hapa kuchangia mnatukatisha katisha.”

Heche amesema leo mnailinda hii kampuni ya Indo Power Solution akihoji zabuni hiyo ilitangazwa wapi? Nani aliyekuwa anafanya mazungumzo ya awali na kampuni hiyo ambayo Gazeti hili la Daily Nation inasema haina hata ofisi Kenya.

“Hivi kama gazeti, mwandishi mmoja anaweza kujua haina ofisi, serikali inashindwa, gavana, mawaziri watano akiwamo Profesa Palamagamba (Kabudi). Yaani gazeti linaweza kuchunguza kuliko serikali nzima,” amehoji Heche

“ Yaani mtu anakuja hapa anasema alikuja na ndege? Mimi na Esther Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini-Chadema) tunakodi helkopita tunakwenda Tarime kwa hiyo sisi ni wafanyabiashara,” amesema Heche

Mbunge huyo amesema Gavana na Profesa Kabudi, “Kama sio rushwa hawawezi kuongoza hata kibanda cha kuuza nyanya.”