Hitimisho la Ndugai, Masele lilijaa kasoro za kiuongozi

Hapana shaka kwamba sakata la mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele na Spika wa Bunge, Job Ndugai, limeshahitimishwa. Japo hitimisho halikukidhi mantiki, ila iliamuliwa ili kufika mwisho. Huko ndiko kukubaliana kutokubaliana.

Masele aliomba radhi kwa Ndugai, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli na wabunge wote. Pamoja na hayo, alikana makosa yote aliyokutwa nayo hatia. Alisema anatamani rekodi za Bunge, kuhusu mazungumzo yake kwenye Kamati ya Maadili iwekwe wazi kila mtu asikie.

Hukumu

Kamati ya Maadili ilimtia hatiani Masele kwa makosa mbalimbali, likiwamo la kugonganisha mihimili ya dola. Ikapendekeza afungiwe mikutano mitatu ya Bunge.

Ndugai akasema Bunge limsamehe Masele na kumpuuza. Hivyo, Bunge likamsamehe. Ndugai hakuishia hapo, akazungumza maneno ambayo yalikuwa nje ya mashtaka dhidi ya Masele.

Kwa kutaka kueleweka vizuri, naomba nikumbushe sakata lenyewe. Masele ni mbunge katika Bunge la Afrika. Vilevile ni ndani ya Bunge la Afrika, ni makamu wa kwanza wa Rais na mkuu wa utawala.

Katika Bunge la Afrika, kuna tuhuma za rushwa na unyanyasaji wa kingono zinazomkabili Rais wa Bunge hilo, Roger Dang. Kamati iliundwa na kumtia hatiani Dang.

Masele alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha tuhuma hizo zinapatiwa ufumbuzi. Inadaiwa Dang alimshtaki Masele kwa Ndugai, maana mbunge katika Bunge la Afrika lazima atoke katika Bunge la nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU). Hivyo Ndugai ni mamlaka ya Masele.

Imebainika kuwa Ndugai alimwandikia barua Dang, ambayo Masele alidai kwamba ingeweza kutumiwa kumvua ubunge wa Bunge la Afrika.

Masele alisema, alijiona kwamba Ndugai alimhukumu bila kumsikiliza, ndiyo maana alitafuta haki kwa kuzungumza na Rais Magufuli, si kama Rais, bali mwenyekiti wa CCM. Alimlalamikia pia Majaliwa, si kama Rais, bali mwenyekiti wa kamati ya wabunge wa CCM. Ndugai na Masele ni wabunge wa CCM, hivyo alitafuta haki kwenye chama.

Magufuli ni mkuu wa Serikali, Majaliwa ni mtendaji mkuu wa Serikali na Ndugai ni mkuu wa Bunge. Sasa basi, kitendo cha Masele kuwalalamikia Magufuli na Majaliwa kwa masuala ya kibunge, Ndugai aliona ni kugonganisha mihimili ya Serikali na Bunge.

Masele analalamika kuwa Ndugai aliandika barua katika Bunge la Afrika ambayo ingeweza kutumiwa na Rais Dang kumvua ubunge.

Anacholalamikia Masele ni kwamba Ndugai alimhukumu bila kumsikiliza.

Mtu akiona kiongozi wake hajamtendea haki inabidi apande ngazi za juu. Spika hana bosi bungeni. Yeye ndiye mkuu wa mhimili. Masele akatambua ipo mamlaka ya chama chake. Shida ni kuwa mabosi wa chama ndiyo mabosi wa mhimili wa Serikali. Sasa hapa Masele amekosea nini? Tatizo ni la muundo wa mamlaka zenyewe kuwa na kofia nyingi.

Tuje kwenye hitimisho la Ndugai, kwamba Masele asamehewe na apuuzwe. Kumpuuza mtu maana yake ni kusema hana maana. Si kauli ambayo inapaswa kutumiwa na viongozi. Masele ni mbunge, vilevile ni mwakilishi wa nchi katika Bunge la Afrika, haitoshi ni makamu wa kwanza wa Rais wa Bunge hilo. Dunia imeambiwa huyo ni wa kupuuza.

Ndugai alipokuwa anahitimisha hoja ya Masele alisema: “Hatuna ubaya na mtu yeyote ni tabia yako.” Hapa Ndugai alisema Masele amekuwa na mwenendo mbaya.

Akaenda nje ya mada kabisa aliposema kuwa Masele amekuwa akimuomba Ndugai ampatie walinzi wa Usalama wa Taifa, magari makubwa aina ya V8 na nyumba kubwa.

Hili Ndugai alilisema kujenga maudhui kwamba Masele ni mwenye kutaka makuu. Kwamba kwa kuwa ni makamu wa kwanza wa rais wa Bunge la Afrika, amekuwa akitaka nchi imhudumie kama kiongozi mkubwa.

Ndugai akasema: “Acha acha Masele. Mimi hao walinzi wa kukaa mgongoni kwako na ma-V8 natoa wapi? Mwenye mamlaka ni Rais na hajaniambia nikupe. Ndiyo maana niliwaambia acheni habari ya kupigapiga makofi, ushabiki nini.”

Maneno ya Ndugai yalithibitisha bila kuacha shaka kwamba kulikuwa na mgongano wa muda mrefu kati yake na Masele. Na aliingiza hoja ya magari, nyumba na walinzi kuhalalisha kwamba Masele amekuwa na makuu mengi. Zaidi, aliona atumie hoja hiyo kuwatuliza wabunge, ndiyo maana alisema: “Niliwaambia acheni kupiga makofi na ushabiki.”

Tujiulize, je, kosa la Masele lilikuwa kuomba walinzi na magari au kugonganisha mihimili? Hili la walinzi na magari lilizungumzwa na Ndugai katika mwenendo upi wa kesi? Alichokifanya ni sawa na hakimu kuchomekea mshtakiwa jambo nje ya mwenendo wa mashtaka. Hukimu aseme: “Unajua umeshawahi kuniibia hata mimi sema sikutaka kukushitaki.”

Ndugai alionya watu kumpelekea Rais ‘umbea’. Alisema “tunamchanganya. Tunamzeesha. Rais anafanya kazi kubwa sana.”

Hapa Ndugai anajishusha mwenyewe kuwa Rais ni wa juu yake. Kama Ndugai mwenyewe anajiweka hivyo, kosa la Masele ni lipi kumshtaki kwa Rais. Ndugai anatakiwa kujipambanua kama kiongozi wa mhimili na heshima ifuate mkondo wake.

Mwisho, ukipitia maelezo ya Masele unaona kuna kitu kati yake na Ndugai. Vilevile hitimisho la Ndugai linadhihirisha kwamba kuna kitu ndani yake kuhusu Masele, tena ni cha muda mrefu. Mpaka hapo, ipo wazi kwamba Masele hakuona kama Ndugai angeweza kumtendea haki.

Wanasheria wana msemo wao wa Kilatini: “Nemo judge in causa sua.” Ambao tafsiri yake ni kuwa hakuna ambaye anaweza kuhukumu kesi yake mwenyewe.

Upo mwongozo wa kisheria unaitwa “Recusal”, kwa maana ya kujitoa kwa jaji, hakimu au mwendesha mashtaka katika shauri ambalo ana masilahi nalo au lolote atakaloshindwa kubaki katikati na kutoa mizania sawa.

Ukipitia kesi ya Masele ilivyoanza hadi kuhitimishwa kwake, utaona Ndugai alishiriki kuhukumu kesi ambayo alishaonesha masilahi nayo. Hata alipoombwa kujitoa ili kuepusha mgongano, aligoma.

Kesi ya Masele na ilijaa kasoro za kiuongozi, hasa jinsi ambavyo Ndugai alihitimisha kwa kuingiza mambo ambayo hayakuwamo katika kesi ya msingi.

Zaidi, Masele ameona hajatendewa haki na Ndugai hakuona busara za kujiweka kando na mchakato wa kesi ili kufanya haki ionekane ikitendeka.