UKAGUZI WA FEDHA ZA UMMA: Hivi ndivyo maendeleo yanavyokwama-CAG

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekuwa akifuatilia kwa karibu kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo kila anapokuwa ziarani.

Jana akiwa Makambako alipokea kilio cha tatizo la mradi wa maji alilolikabidhi kwa mkuu wa mkoa, ikiwa ni siku moja baada ya kupokea tatizo la kuchelewa kukamilika kwa kituo cha basi cha Njombe. Lakini sasa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaweza kumpa mwanga zaidi.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni juzi, inaonyesha kuwa halmashauri 185 zilikuwa na kasoro tofauti katika kukusanya fedha kutoka vyanzo vyake, kupanga miradi ya maendeleo, kuisimamia, kuigharimia na pia hazikupokea fedha kulingana na mahitaji.

Mamlaka nyingi za Serikali zimeendelea kukusanya mapato chini ya makadirio, ukiacha mamlaka 34 ambazo zilimudu kukusanya jumla ya Sh140.2 bilioni, sawa na asilimia 13 zaidi,” anasema CAG Profesa Mussa Assad katika ripoti yake.

“Hata hivyo, kwa ujumla kulikuwa na makusanyo ya chini ya makadirio ya Sh111.2 bilioni, sawa na asilimia 16,” anasema CAG.

Lakini halmashauri zilizopewa fedha zaidi ya bajeti zao za miradi ya maendeleo zilikuwa 23 na zilipokea jumla ya Sh22.06 bilioni, wakati zilizozidishiwa fedha za matumizi zilikuwa 20 na zilipewa jumla ya Sh42.6 bilioni.

“Bila ya kuwepo bajeti ya ziada iliyopitishwa, utoaji wa fedha zaidi unaweza kuweka mazingira ya matumizi mabaya au wizi,” inasema taarifa hiyo.

Ripoti hiyo inataja usimamizi dhaifu wa miradi ya maendeleo, kuachwa kwa muda mrefu kulisababisha miradi yenye thamani ya Sh52.4 bilioni kutokamilika.

“Tathmini niliyofanya kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo nimebaini kuwa fedha za utekelezaji hazikutoka kwa wakati,” anasema CAG Mussa Assad katika ripoti hiyo.

“Ushiriki usioridhisha wa jamii kwenye shughuli za miradi, usimamizi usioridhisha wa miradi na kutelekezwa kwa miradi kwa muda mrefu kumesababisha kuwapo kwa miradi ambayo haijakamilika.”

Pia halmashauri 45 hazikutekeleza miradi iliyopangwa kutokana na kutopokea fedha kutoka Serikali Kuu ambazo zilikuwa jumla ya Sh41.5 bilioni.

Alishauri uongozi wa halmashauri hizo 47 kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inatekelezwa na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa; kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa miradi inayotekelezwa katika ngazi ya Kata na kijiji.

Pia, aliishauri Wizara ya Fedha kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ili kuziwezesha halmashauri kutekeleza na kukamilisha miradi iliyopangwa kwa wakati.

Pia CAG amebaini miradi 27 katika halmashauri 16 yenye thamani ya Sh5.2 bilioni ambayo imekamilika, lakini haifanyi kazi.

Pia fedha kwa ajili ya wanawake na vijana ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, hazikupelekwa kwa wahusika katika halmashauri 142, wakati zile zilizopelekwa, hazikurudishwa.

Pia halmashauri 62 hazikupeleka fedha zinazofikia Sh3.3 bilioni katika vijiji na kata.

Suala la kuchelewa kwa miradi ya maendeleo liliibuka pia bungeni jana wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Tamisemi.

Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche alisema kutotolewa kwa fedha hizo katika sekta mbalimbali za kilimo, afya na maji ni kiashiria cha masuala ya maendeleo kulala.

Heche alitoa mfano wa Wizara ya Viwanda ambayo ilitengewa Sh90 bilioni lakini imepewa Sh5.4 bilioni tu, akisema kwa kitendo hicho wizara haiwezi kufanikisha ajenda ya Serikali ya kuunda uchumi wa viwanda.