VIDEO: Hivi ndivyo mfanyabiashara aliyetajwa na Magufuli alivyowazungusha TRA, kugoma kuwapa rushwa

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana Jumamosi Juni 7, 2019 alitumia sehemu ya hotuba yake katika mkutano wa Rais John Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Wilaya zote nchini Tanzania, kueleza sakata la mfanyabiashara aliyegoma kuwapa rushwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kuushikilia mzigo wake tangu mwaka 2017.


Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana Jumamosi Juni 7, 2019 alitumia sehemu ya hotuba yake katika mkutano wa Rais John Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Wilaya zote nchini Tanzania, kueleza sakata la mfanyabiashara aliyegoma kuwapa rushwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kuushikilia mzigo wake  tangu mwaka 2017.

Majaliwa wakati akijibu baadhi ya changamoto za kufanya biashara zilizotolewa na wafanyabiashara hao, alieleza sakata la maofisa hao watatu wa TRA wanaotuhumiwa kuomba rushwa kwa mfanyabiashara huyo.

Kutokana na maelezo hayo ya Majaliwa, Rais Magufuli alimuagiza mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Diwani Athuman kuwakamata watumishi hao na kuwapeleka mahakamani.

Katika maelezo yake Majaliwa amesema mfanyabiashara huyo alikamatwa na mizigo yake mwaka 2017 na kurudishiwa mwaka 2019 baada ya yeye kuingilia kati.

“Rais kuna mfanyabiashara mmoja mizigo yake imekamatwa mwaka 2017 ndio tumeirudisha juzi kwa sababu tu aliyemkamata aliomba rushwa ila mfanyabiashara alikuwa makini akagoma kutoa rushwa akakubali mzigo ukae huko.”

“Alivyokuja kueleza tukagundua ni kweli alikuwa ameonewa,” amesema Majaliwa.

Wakati Majaliwa akieleza sakata hilo alikatishwa na Rais Magufuli akihitaji kupata majina ya watumishi hao watatu.

Kamishna wa ndani wa TRA alitakiwa kuwataja watu hao na kubainisha kuwa hatua zimanza kuchukuliwa  huku akieleza kutoyakumbuka vyema majina yao.

 “Basi hao watatu wote kamishna wa Takukuru hakikisha unawaweka ndani harafu wapelekwe mahakamani.”

“Watakapokuwa mahakamani kamishna wa TRA uwe umewasimamisha kazi, na TRA mkapige hesabu ile biashara yake imekaa kwa miaka mitatu ili mumlipe fidia,” amesema Magufuli.

Alivyokwepa kutoa rushwa

Majaliwa amesema mfanyabiashara huyo alikuwa anatoka Zambia akiwa amefunga biashara na kupita maeneo yote ya ukaguzi na nyaraka zake zote kuonekana kuwa sawa.

“Alipofika Kimara alikutwa na tatizo ambalo lilikuwa ni kukataa kutoa rushwa usiku ule. Baada ya kukataa kutoa rushwa mfanyabiashara huyo alikubaliana na watumishi hao kuelekea Kariakoo nyumbani kwake kwa ajili ya kupata hicho walichokuwa wanakitaka.”

“Baada ya kufika nyumbani mfanyabiashara huyo aliingia ndani na kujifungia yeye na dereva wake na kuwaeleza watumishi hao kuwa hana mpango wa kuwapa rushwa wakitaka wamuue na gari lake wachukue,” amesema Majaliwa.

Amesema wakati mfanyabiashara na watumishi hao wa TRA wakirushiana maneno, lilipita gari la polisi na maofisa hao kuchukua mzigo huo na kwenda kuufungia mzigo huo.

“Inaelezwa mfanyabiashara huyo alifika ofisini kwao (TRA) kwa ajili ya kufuatilia mzigo huo na aliwakuta wadada wawili ambao wote walimgombania wakihitaji kumsaidia ndipo ulipofanyika ukaguzi na kubainika kuwa alikuwa ameonewa kwa mizigo yake kukamatwa kwa miaka mitatu,” amesema Majaliwa.