Askofu: Hofu ya Mungu itatupa Katiba

Monday May 19 2014

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akiongoza watu mbalimbali kumpongeza Askofu Mkuu mpya wa Jimbo la Songea, Damian Dallu katika Kanisa la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba mjini Songea jana. Picha na Joyce Joliga 

By Joyce Joliga, Mwananchi

Songea. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu amesema Katiba Mpya itapatikana iwapo wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa na maadili ya kiroho kwa kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu bila kupindisha ukweli wa mchakato wa maoni ya Katiba.

Amesema kupotosha ukweli wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba unaweza kuipeleka nchi kubaya.

Hayo aliyasema jana katika Ibada maalumu ya kumsimika rasmi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Mathias Mulumba lililopo Mjini Songea ambayo ilihudhuriwa na maelfu ya waumini, viongozi wa chama na Serikali, viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.

Askofu Dallu alisema wapo watu wanaodhani kuwa iwapo Katiba Mpya itapatikana matatizo yao yatakwisha kitu ambacho hakina ukweli kwa madai kuwa hata Katiba iliyopo imeongoza nchi kwa miaka 50 na watu waliungana kiroho na siyo kwa kupitia makaratasi ambayo yanaweza kuchakachuliwa.

Alisema Watanzania hawana budi kumwomba Mungu asaidie kupata viongozi watakaoweza kuliongoza taifa kuanzia ngazi za chini hadi juu kwa kufuata maadili ili nchi isije ikaiingia kwenye machafuko.

Akitoa salamu za Mkoa wa Ruvuma Mkuu wa Mkoa, Said Mwambungu alisema kuwa Serikali itatoa ushirikiano kwa askofu huyo katika kuunga mkono juhudi na mafanikio yanayofanywa na Kanisa Katoliki katika kutoa huduma zake kwenye Sekta ya afya, elimu, kilimo na maji.

Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na viongozi wa dini ambao walikuwa wakijituma kwa bidii kusaidia wananchi bila kujali madhehebu wanayotoka kitu ambacho kimeipa Serikali faraja na inaomba ushirikiano huo kuendelea.

Spika Makinda akitoa salamu kwa niaba ya Serikali amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii badala ya kuitegemea Serikali au kanisa kuwaletea maendeleo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo binafsi.

Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Tarcisius Ngalalekumtwa amempongeza Askofu Dalu kwa kukubali kushika nafasi hiyo na kukemea tabia za wizi na mauaji kuwa ni kinyume cha matendo ambayo hayampendezi Mungu.

Alisema dhamira safi, upendo na wema, upole, ukarimu na rehema ndiyo matunda na zabibu za kumtolea Mwenyezi Mungu

Advertisement