Hoja tano zatawala maoni ya wananchi, taasisi kuhusu muswada wa vyama vya siasa

Dodoma. Wananchi na taasisi mbalimbali wametoa maoni kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, wakijikita zaidi katika mambo matano.

Walitoa maoni hayo juzi na jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria jijini Dodoma kazi ambayo itaendelea leo kwa vyama 16 vya siasa.

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Kayumbu Kabutale alisema jana kwamba watashiriki katika utoaji wa maoni hayo huku Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema chama hicho pia kitawasilisha maoni yake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Mohamed Mchengerwa alitaja maeneo hayo matano ambayo yaligusiwa zaidi na watoa maoni kuwa ni ruzuku za vyama vya siasa, mamlaka ya msajili hasa kipengele cha kuwa na uwezo wa kukifuta chama, kuwapo au kutokuwapo kwa vikundi vya ulinzi ndani ya vyama.

Mengine ni vyama kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, idadi ya wanachama katika utaratibu wa kusajili chama na mtu anayepaswa kusajili chama yeye na wazazi wake wote wawe raia wa Tanzania, huku Mchengerwa akisema kuwa waliotoa maoni juzi walikuwa 220 na jana walitarajiwa kusikiliza wengine 300.

“Haya ni mambo ambayo yameleta ubishani mkubwa na sisi kama kamati tutapitia hoja zote na kuona yale ambayo ni ya msingi katika utungaji wa sheria ambayo itakuwa nzuri. Eneo ambalo litabainika kukiuka Katiba hatutakwenda nalo,” alisema Mchengerwa.

Ingawa hakufafanua, alisema kamati itachukua maeneo ambayo yamezingatia Katiba ili kutunga sheria ambayo haitaenda kupingwa mahakamani.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, wakili wa kujitegemea, Nashon Nkhungu alitaja kipengele chenye ukakasi kuwa ni cha tano A ambacho kina sehemu ya elimu ya uraia ambayo msajili wa vyama vya siasa anapewa mamlaka ya kuelezwa elimu ya uraia inayofundishwa na taasisi au chama inahusu nini na inalenga kupata faida gani.

Kwa mamlaka hayo, alisema msajili anaweza kakubali au kukataa akitoa sababu ikiwamo ya kuleta matokeo mabaya huku akiwa ndiye mwamuzi wa mwisho wa nani apewe elimu ya uraia na nani asipewe.

Pia alisema, “Kifungu cha tatu kinaeleza kuwa asasi za kiraia chama cha siasa ambacho hakitafuata utaratibu huo vitakuwa vimefanya kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini siyo chini ya Sh1 milioni au isizidi Sh5 milioni na kifungo kuanzia miezi sita na kisizidi miezi 12 na anaweza kupata vyote au kimojawapo,” alisema Nkhungu.

“Adhabu kwa vyama vya siasa vitakavyokiuka itakuwa kubwa kidogo. Watalipa faini ya kati ya Sh5 milioni hadi Sh30 milioni.

Alisema kifungu cha 5 B kinampa msajili nguvu za kuhitaji taarifa yoyote anayoihitaji kutoka kwenye chama chochote cha siasa ili kutimiza majukumu yake.

“Chama kisipotimiza kitatozwa faini isiyopungua Sh1 milioni na haitakuwa zaidi ya Sh10 milioni na mtu ambaye anapaswa kutoa hizo taarifa na hakufanya hivyo atatozwa faini siyo chini ya Sh1 milioni na haitazidi Sh3 milioni au kifungo kuanzia miezi sita na hakitazidi mwaka mmoja.”

Alisema kifungu cha sita kimempa nguvu msajili wa vyama kutoguswa na mtu yeyoye ay hata mahakama.

Mwitikio wa kutoa maoni

Mchengerwa aliwaambia wanahabari kuwa wananchi wengi walijitokeza kutoa maoni yao kuhusu muswada huo idadi ambayo alisema hajawahi kuishuhudia katika kipindi cha chote alichokaa ndani ya kamati hiyo.

Alisema kutokana na wingi wa watu imewalazimu wengine kuwahudumia jana.

“Jumatatu na Jumanne tutaipitia michango yao ili kuona ni ipi itafaa tuitungie sheria itakayoweza kudumu kwa miaka 50 au 100 ijayo,” alisema.

Alisema leo vyama 16 vyenye usajili nchini vitatoa maoni yao kuhusu muswada huo na Baraza la Vyama vya Siasa nalo litatoa maoni yao kesho.

Mmoja wa wananchi waliotoa maoni katika kamati hiyo, Fabian Ronatus alitaka waanzilishi wa vyama kulazimika kuwa ni raia Tanzania wao na wazazi wao ili kuepuka kuhamisha itikadi na tamaduni kutoka mataifa mengine.

Mwananchi mwingine, Matha Ngoiko alitaka suala la ulinzi kubakia kwa majeshi yaliyopo kisheria na kuondokana na vyama vya siasa kuwa na vikundi vyama vya ulinzi.