Hoja ya wabunge kuichangia Yanga yakwama bungeni

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy akiomba muongozo bungeni jijini Dodoma leo, alipokuwa akiomba Klabu ya Yanga ipatiwe msaada na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) unaofanya kazi ya kusaidia kaya maskini ili iweze kujinasua kwenye na ukata wa fedha unayoikabili klabu hiyo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

 Leo Ijumaa Aprili 5, 2019 mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy ameomba mwongozo bungeni akitaka wabunge kuichangia klabu ya Yanga, hoja ambayo wabunge waliikataa.

 

Dodoma. Mwongozo ulioombwa bungeni jijini Dodoma na mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy akitaka wabunge kuichangia klabu ya Yanga umekwama baada ya wawakilishi hao wa wananchi kupinga hoja hiyo.

Keissy ameomba mwongozo huo leo asubuhi Aprili 5, 2019 baada ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuitambulisha kamati ya kuhamasisha kuichangia Yanga ya jijini hapa iliyoalikwa kutembelea Bunge.

Kessy amesema kutokana na uwepo wa kamati hiyo, ni vyema likapitishwa kapu bungeni ili wabunge waweze kuichangia klabu hiyo ambayo jana ilitoka sare ya bao 1-1 na Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Kessy amezungumza kuhusu kuichangia Yanga na mwongozo wake anazungumzia kapu kuletwa hapa (bungeni) kulingana na matangazo yaliyopo. Kwa kuwa wote tunamfahamu Keissy kuhusu mchango tumkubalie kwa maana tukatwe fedha ili,” amesema Dk Tulia  ambaye alishindwa kumalizia kauli yake kutokana wabunge kuanza kupaza sauti, kuzungumza bila kufuata utaratibu.

“Wabunge tusikilizane, naomba tusikilizane waheshimiwa wabunge, nimeombwa mwongozo hapa na hili jambo linahusu wabunge kuridhia kwa mujibu wa Keissy na pendekezo lake.”

Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka akilalamika bungeni kufuatia wabunge wengi kupinga kukatwa posho zao ili kuchangia Klabu ya Yanga, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Baada ya wabunge kutulia, Dk Tulia alilihoji Bunge kuhusu hoja hiyo ya Keissy, “Wabunge walio tayari kuchangia waseme ndio na wasio tayari waseme sio.”

Kutokana na wabunge wengi kusema sio, Dk Tulia amesema waliokataa hoja hiyo ni wengi zaidi, hivyo haijapitishwa.

Wabunge hao walisikika wakisema wanaweza kukatwa Sh50,000 au Sh100,000 katika posho zao ili kuichangia Yanga huku Keissy akitamka Tasaf (Mpango wa Kusaidia Kaya Masikini).