Huduma ya TTCL hakiki kusaidia wakulima kujua ubora wa mbegu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Waziri Kindamba mara baada ya kuwasili katika eneo la utoaji wa Gawio katika ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Ili kuwasaidia wakulima kampuni ya TTCL inatarajia kuanzisha huduma ya TTCL hakiki itakayomsaidia mkulima kuhakiki ubora wa mbegu kabla ya kupanda

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amesema katika kuwasaidia wakulima kampuni hiyo inatarajia kuanzisha huduma ya TTCL hakiki itakayomsaidia mkulima kuhakiki ubora wa mbegu kabla ya kupanda.

Ameyasema hayo leo Jumanne Mei 21, 2019 katika hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali iliyoenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma ya video conference.

Amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais John Magufuli juu ya kampuni hiyo kutafuta namna inavyoweza kuwasaidia wakulima.

“Kwa kutumia ‘code’ au ‘app’ mkulima ataweza kuhakiki ubora wa mbegu kuanzia Julai mwaka huu na hii itafanikisha katika kuzisaidia mamlaka kudhibiti mbegu, kufanya bei za mbegu kuwa nafuu sokoni, kuondoa mbegu bandia sokoni.”

“Namna ya kutumia, mkulima atafungua app ataweka code ya uhakiki wa mbegu katika app au kwa kutumia qrcode iliyo katika code ya uhakiki wa mbegu, mkulima atapiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupata taarifa wanayostahili.”

Mbali na hilo pia alizungumzia suala la baadhi ya watu kupinga maendeleo anayofanya Rais John Magufuli amesema ni hulka yao ndiyo maana hata Yusuph asingeweza kufikia utawala kama asingetupwa katika shimo.

Amesema kupingwa ni changamoto ambazo zipo katika uongozi huku akimuomba kuendelea kuzivumilia wakati nchi inapiga hatua kuelekea maendeleo makubwa.

“Daudi asingeweza kuwa mfalme bila ya kupambana na Goliath na Yesu asingeweza kuleta ukombozi bila ya kusalitiwa na Yuda.”