Huu ndio mji wa Serikali Mtumba

Mtumba ni neno linalobeba jina la mti wenye matunda ambao hustawi katika mikoa ya Dodoma na Singida na sehemu ya mkoa wa Manyara.

Mti huu hupevusha matunda yake Oktoba kipindi ambacho ni cha ukame kwa maeneo hayo lakini, mti wake ukiwa mbichi hutumika kwa ajili kuleta harufu nzuri kwenye maziwa baada ya kuuchoma na kutia kwenye maziwa hayo.

Kwa wenyeji wa mkoa wa Dodoma (wagogo), pia huutumia kubashiri kama msimu wa mvua umekaribia, hivyo msimu wa matunda ya mti huu ndio hufungua maandalizi ya kusafisha mashamba na kuezeka nyumba za matembe.

Jina la mti huo ndilo lililobeba Kijiji cha Mtumba ambacho kwa sasa kinaweka historia kubwa ya Tanzania baada ya ndoto ya miaka 46 ya Serikali kuhamia Dodoma ilipotimia hivi karibuni.

Kijiji hiki kipo umbali wa kilomita 17 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma na kilomita 12 kutoka Ikulu ya Chamwino.

Serikali imehamia Dodoma, ofisi za wizara zote ziko Mtumba, huduma za kiserikali zinapatikana Mtumba, sasa ni Mtumba kwa kila kitu. Ndoto ya Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1973 sasa imetimia.

Tangu tamko la kuhamia Dodoma lilipotolewa, ilimchukua Nyerere miaka 12 akiwa madarakani lakini hakufanikiwa, akafuata Mzee Ali Hassan Mwinyi (1985 -1995), akafuata Benjamini Mkapa (1995-2005), kisha mtangulizi wa Rais John Magufuli, Jakaya Kikwete (2005-2015) lakini kila mmoja alitamka bila mafanikio.

Serikali ya awamu ya tano iliyoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015, ilianza kuhamia Dodoma tangu mwaka 2017 lakini wizara nyingi zilihamia katika majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) umbali wa kilomita 10 kutoka katikati ya jiji.

Novemba mwaka jana, eneo la Mtumba liligeuka lulu ghafla baada Serikaki kulivamia kama nyuki na majengo kuanza kuota kama uyoga hivyo kutoa fursa kwa wakazi wa Mtumba na Jiji la Dodoma ambao walipata ajira lukuki.

Muda waliopewewa wajenzi wa majengo hayo ulikuwa miezi mitatu kabla ya kuongezwa muda kidogo, sasa karibu majengo ya wizara zote 23 yameshachukua wafanyakazi kwa ajili ya kuanza shughuli za Serikali.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alizindua mji huo na kuagiza majengo ambayo hayakuwa yamekamilika watumishi wake wahamie haraka hata kama ni kwenye miembe jambo ambalo limetekelezwa kikamilifu.

Pole sana kwa waliohamia kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo yao na hasa ofisi ya Rais (Tamisemi) ambayo ujenzi wake bado kabisa licha ya kujipa tumaini kuwa kazi itakamilika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu tu.

Hali ilivyo Mtumba

Wingi wa magari hasa ‘mashangingi’ yanaonyesha utofauti mkubwa katika eneo hilo na kuimarika kwa ulinzi kunakofanya wenyeji kuona kuna jambo katika eneo hilo.

Ukweli ni kuwa, bado kuna malori ya mchanga na mawe ambayo yanaingia katika eneo hilo, vibanda vya mabati bado vimeupamba mji wa kiserikali na miungurumo mingi ya magari makubwa yanayopeleka vifaa.

INAENDELEA UK 22

INATOKA UK 21

Mazingira hayajaboreshwa licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika eneo hilo ambazo kwa sehemu kubwa zimeanza kuzaa matunda na hasa ukarabati wa barabara za mzunguko katika mji huo zenye urefu wa kilomita 35.

Kwa sasa bado kuna mkanganyiko katika kuzifikia wizara, maeneo hayajazoeleka, wengi hawajui wapitie wapi kufikia maeneo husika licha ya vibao vidogo kuwekwa katika kila kona ya barabara inayoingia kwenye eneo la wizara.

Huduma muhimu

Bado hakuna maduka, hakuna migahawa, hakuna hata sehemu za karibu za kununua vocha kwenye maeneo hayo.

Katika eneo hilo pia kunapaswa kuwepo walau kituo kidogo cha polisi kwa huduma za dharura hasa kuwakabili wahalifu ambao hupenda kujipenyeza katika maeneo ambayo hutolewa huduma kama wizara.

Serikali imeahidi kujenga kituo kikubwa cha afya kwa kutenga Sh4 bilioni kitakachotumika hata kwa wakazi wanaoishi kuzunguka eneo hilo hasa vijiji vya Mtumba, Ihumwa, Mahomanyika, Vikonje na Mahomamakulu.

Wahusika wa masuala ya usafiri ikiwamo Sumatra wanapaswa kuainisha kwa mapana kuhusu safari za magari ya abiria kwani licha ya kuwa wamesharuhusu safari za huko, lakini hakuna ainisho la safari wapi zinakoishia.

Mbali na safari za ndani, lakini suala la kutenga stendi walau ya muda katika eneo la Mtumba ili kuwarahisishia watu wanaosafiri kutoka mikoa ya mbali waweze kushukia hapo kuwahi huduma badala ya kulazimika kwenda hadi eneo la Nzuguni iliko stendi ya mkoa.

Fursa zilizopo kwa sasa

Kuwepo kwa usafiri wa bajaji, pikipiki na taksi linaweza kuwa jambo la muhimu kwa sasa kuliko mambo mengine kutoka njiapanda ya barabara kuu ya Morogoro–Dodoma kuingia ndani ya mji wa kiserikali ambako ofisi zingine zinafikia zaidi ya kilomita tatu kutoka barabara kuu.

Ipo fursa ya kuweka “stationary” kwa ajili ya shughuli za kiofisi kwa wanaohitaji kudurufu na huduma zingine wanazozifuata. Pia ipo fursa ya kuweka migahawa kwa kuwa huduma ya chakula ni jambo lisilokwepeka kwa wale watakaokakuwa eneo kwa muda mrefu wakifuatilia huduma mbalimbali.

Majengo mengine yapendezesha mji

Ni ukweli kuwa, majengo yaliyokamilika yameanza kuupendezesa mji wa kiserikali ambao unapambwa pia na vilima viwili vinavyouzunguuka na miinuko midogo.

Mfano wa majengo yaliyokamilika na mandhari yake kuwa katika hali nzuri, ya kuvutia ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara za Maliasili na Utalii, Fedha, Utumishi na Utawala bora na majengo mengine yaliyotawanyika.

Udom itapumua

Wakati ofisi za Serikali zilipohamia Chuo Kikuu cha Dodoma, kuliibuka madai ya kuhamishia msongamano wa watu katika eneo la chuo na kuibua hofu kuhusu usalama wa wanafunzi na hasa watoto wa kike dhidi ya wanaume wakware.

Kwa utaratibu huu, Udom itapumua na msongamano wa magari kuingia na kutoka utapungua, hivyo shughuli za chuo zitakuwa katika hali yake stahili.