Huu ndio msimamo wa Waislamu Tanzania kuhusu uzazi wa mpango

Muktasari:

Baraza Kuu la Waisalimu Tanzania (Bakwata) limezungumzia uzazi wa mpango huku likitoa tamko kuhusu suala hilo.

Tanga. Baraza Kuu la Waisalimu Tanzania (Bakwata) limetoa tamko kuhusiana na ushiriki wake katika kampeni ya uzazi wa mpango, likitoa masharti matano yanayokubalika kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.

Tamko hilo lilitolewa jana Jumanne Aprili 16, 2019 na Baraza la Maulama la Bakwata katika semina ya viongozi wa dini ya Kiislamu iliyofanyika jijini Tanga chini ya ufadhili wa mradi wa uzazi wa mpango (AFP).

Akisoma tamko hilo, mara baada ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir kueleza hitilafu za wanazuoni wakubwa duniani wa Kiislamu kuhusu uzazi wa mpango, Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga alisema suala la riziki au uchumi kulihusisha na uzazi wa mpango halikubaliki kwa mujibu wa sheria za Kiislam.

Alizitaja sababu tano zinazokubalika kwa mujibu wa dini ya Kiislamu kuwa ni kuchunga uzuri wa afya ya mke na kuyalinda maisha yake na hatari ya uchungu na uzazi na mengine.

Alisema utaratibu wa uzazi wa mpango unawataka wazazi kuwanyonyesha watoto wao miaka mwili, utaratibu ambao unatoa fursa kwa watoto kunyonya vizuri bila kughasiwa.

“Katika kipindi hicho, mwanamume atalazimishwa kuhakikisha mama anapata chakula cha kutosha na mavazi,” alisema Sheikh Chizenga.

Mbali na hayo, alisema  suala la uzazi wa mpango linatakiwa kuzingita afya ya mtoto, haki za mtoto, afya ya mama, haki za mama, malezi, maslahi ya mtoto, masuala ya kuhakikisha yanazingatiwa.

Kuhusiana suala la riziki au uchumi kulihusisha na uzazi wa mpango, alisema baraza hilo limekubaliana kwamba halikubaliki kwa mujibu wa sheria za Kiislam.

Kwa upande wa  mimba za utotoni kwa mtoto wa kike, baraza hilo limesema msishana  atakuwa tayari kwa kuolewa pale anapo balehe.

“Lakini kwa mujibu wa kanuni iwapo atathibitika na daktari mwadilifu kwamba umri alionao akiolewa anakuwa kwenye hatari iwapo anapobeba ujauzito, sheria inazuia msichana huyo asiolewe,” alisema  Sheikh Chizenga.

Alisema mtoto wa kike aliyebalehe atakapohofiwa kuingia kwenye uchafu

wa zinaa baada ya kubalehe, kwa mujibu wa dini ya Kiislamu kuolewa

itakuwa ni wajibu kwake.

Akizungumza katika semina hiyo, Mufti Zuberi alisema  uzazi wa mpango

ni masuala yaliyozungumziwa sana na wanazuoni wa elimu ya sheria ya

Kiislamu tokea enzi hizo za maswahaba juu ya suala hilo.

Aidha, alisema suala hilo la uzazi wa mpango wanazuoni dunia

walitofautiana kutokana na kila mmoja kuwa na uelewa wake, huku

likiwekwa wazi kwa mujibu wa dini ya Kiislamu ambapo inamtaka

mzazi amnyonyeshe mtoto kwa kipindi cha miaka miwili.

Alisema hitaji la mtoto kunyonyeshwa kwa kipindi hicho ni dhahiri

kunampa mwanya mzazi kuimarisha afya yake na mtoto, hivyo suala

hilo lipo na limeshapangwa kwa mujibu wa dini ya Kiislamu na si

vinginevyo.

Meneja Utetezi toka Mradi wa Uzazi wa Mpango AFP, James Mlali

alikiri tafiti zinazofanywa na wanasayansi juu ya masuala uzazi wa

mpango yamemekwisha kuelezwa kwa mujibu wa dini ya Kiislam.

Alisema yapo matatizo yanayoweza kujitokeza iwapo hakutazingatiwa

suala hilo la uzazi wa mpango ikiwamo kutokea athari za

udumavu wa viungo vya mtoto na ubongo.

Mkuu wa Mkoa Tanga, Martin  Shigella alilipongeza baraza hilo kwa kutoa msimamo wake kuhusu uzazi wa  mpango ambao una faida kwa pande zote kijamii.