Huyu ndiye aliyelipa sura jiji la Dar unaloliona sasa

Jiji la Dar es Salaam ni moja kati ya miji mikubwa barani Afrika ambayo inakuwa kwa kasi. Likiwa na idadi ya watu takribani milioni tano, jiji hilo lina majengo mazuri na yakuvutia ambayo yalijengwa kabla na mapema baada ya uhuru.

Maendeleo ya jiji hilo yalitokana zaidi na mapenzi ya wakoloni kuweka makazi yao, hivyo waliboresha miundombinu yake ikiwa ni pamoja na majengo mbalimbali waliyoishi au kuyatumia kama ofisi, shule na kibiashara.

Moja ya watu waliochangia katika kubadilisha sura ya jiji la Dar es Salaam ni Peter Bransgrove, msanifu majengo raia wa Uingereza. Bransgrove amefanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo Kenya na Uganda.

Kwa mara ya kwanza, Bransgrove alifika nchini mwaka 1947 baada ya kumaliza masomo yake katika chuo cha usanifu majengo cha Royal Academy cha Uingereza. Aliajiriwa katika mradi wa kilimo cha karanga huko Kongwa, Dodoma kabla ya kurejea Dar es Salaam mwaka 1948 baada ya mradi huo kwisha.

Alipofika Dar es Salaam alianzisha kampuni yake ya usanifu majengo iliyotambulika kama C.A Bransgrove & Partners. Kampuni hiyo ilikuwa kampuni huru ya kwanza kuanzishwa nchini na iliaminiwa kwa miradi mikubwa ya usanifu.

Msanifu huyo wa majengo ambaye alizaliwa mwaka 1914, alikuwa ni mjumbe wa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kati ya mwaka 1951–1955 na alifanya kazi kama mshauri wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Bransgrove alifanya safari kadhaa kwenda Roma, Italia ambako alikwenda kushirikiana na kampuni ya Whiting Associates International katika kusanifu majengo ya chuo cha tiba cha KCMC kilichopo Moshi, Kilimanjaro.

Bransgrove alitumia mtindo wa majengo ambayo ni stahimilivu katika hali zote za hewa, na aina yake ya ubunifu wa majengo inafahamika kuwa ya kipekee hapa nchini hasa kwa wakati ule ambao teknolojia bado ilikuwa chini.

Amebuni majengo mbalimbali katika mji wa Dar es Salaam zikiwemo nyumba za mabalozi, majengo makubwa ya biashara na ofisi ambayo baadhi yanatumika mpaka sasa lakini mengine yamebomolewa.

Msanifu wa majengo, Aggrey Mbonde anamzungumzia Bransgrove kama mtu aliyeanzisha ubunifu wa majengo yenye mtindo tofauti nchini na kwamba ubunifu wake ulikuwa ukilenga matumizi ya majengo ya muda mrefu.

Anasema sehemu kubwa ya majengo ya yaliyojengwa kabla na hata baada ya kupata uhuru yalikuwa ya kisasa na yaliyotumia teknolojia mpya wakati ule ikilinganisha na iliyokuwa ikitumika awali.

“Nimefuatilia historia yake na kuangalia kazi alizozifanya nikabaini kwamba alileta teknolojia mpya ya usanifu wa majengo hapa nchini. Walikuwepo wasanifu wengine lakini yeye alikuwa na ubunifu wa kipekee,” anasema Mbonde.

Mtaalamu huyo wa majengo anasema Bransgrove alibadilisha muonekano wa jiji la Dar es Salaam kwa kubuni majengo ambayo yaliupamba mji huo tofauti na ulivyokuwa awali kabla ya ujenzi wa majengo aliyobuni.

Mbonde anasisitiza kuwa msanifu huyo anastahili kupewa heshima kwa mchango wake mkubwa katika jiji hilo licha ya kwamba hivi sasa kuna maendeleo ya teknolojia ya usanifu wa majengo tofauti na aliyoitumia wakati ule.

“Kwa sasa kuna maendeleo makubwa ya usanifu wa majengo kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia. Hata hivyo, ubunifu wa Bransgrove una maana kubwa kwa sababu alifanya kazi kubwa ambayo kwa wakati ule teknolojia ilikuwa bado iko chini,” anafafanua mtaalamu huyo.

Kwa upande mwingine anahamasisha wasanifu wa sasa kuwa na ubunifu zaidi ambao utazifanya kazi zao ziweze kudumu kwa muda mrefu na kukumbukwa na vizazi vijavyo.

Majengo maarufu aliyoyasanifu

Moja ya majengo maarufu yaliyosanifiwa na Bransgrove ni jengo la Hifadhi (Hifadhi House). Jengo hilo lipo katika Mtaa wa Azikiwe karibu na Sanamu ya Askari, katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Ujenzi wa jengo hilo linalotumika kibiashara na kiofisi ulikamilika mwaka 1961 na kukarabatiwa tena mwaka 1999.

Jengo jingine ni Luther House ambalo linamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Jengo hilo ambalo ujenzi wake ulikamilika mwaka 1963 linapatikana katika Barabara ya Sokoine na linatumika kama ofisi na hoteli.

Bransgrove alibuni pia jengo linalotumiwa na Benki ya NMB, Mtaa wa Samora. Ujenzi wa jengo hilo ambalo zamani lilitumika kama Benki ya Barclays ulikamilika mwaka 1955, hata hivyo limekuwa likikarabatiwa kila baada ya muda fulani.

Pamba House ni moja ya kazi za Bransgrove, jengo hilo linapatikana Garden Avenue katika Barabara ya Pamba. Ujenzi wake ulikamilika mwaka 1958 likiwa na ghorofa mbili lakini liliongezwa na kukamilika mwaka 1962 likiwa na ghorofa tano zilizopo mpaka sasa.

Msanifu huyo alibuni pia jengo la YWCA lililopo Mtaa wa Azikiwe, mkabala na Kanisa la Anglikana la Mt. Albano. Jengo hilo lilikamilika mwaka 1969 na linatumika kwa biashara na hoteli.

Bransgrove alibuni pia jengo la posta lililopo katika Mtaa wa Azikiwe ambalo ujenzi wake pia ulikamilika mwaka 1969. Jengo hilo linalomilikiwa na Serikali linatumiwa na Shirika la Posta nchini.

Shule ya Msingi Bunge pia ina majengo yaliyosanifiwa na Mwingereza huyo. Awali jengo hilo lilijulikana kama Junior European School. Shule hiyo ilijengwa mwaka 1957 ikimilikiwa na Mamlaka ya Elimu ya Wazungu (EEA) ikiwa ni maalumu kwa watoto wa wakoloni.