VIDEO - IGP Sirro amlilia Mengi

Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP) Saimon Sirro akisalimiana na  mtoto wa Mzee Mengi Abdiel Mengi baada ya kuwasili msibani katikikati ni Deogratius Liyunga.

Muktasari:

 

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amezungumzia aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi kuwa alikuwa mtu aliyejishusha kwa watu wote licha ya kuwa na fedha. Pia amesema polisi wanafuatilia kwa karibu habari zinazosambazwa kuhusiana na kifo hicho

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amezungumzia aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi kuwa ni mtu alijishusha kwa watu wote licha ya kuwa na fedha.

Mengi ambaye ni mfanyabiashara maarufu Tanzania aliyewekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo tasnia ya habari na viwanda, alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, akiwa Dubai, Falme za Kiarabu.

Sirro ametoa kauli leo Jumamosi Mei 4 muda mfupi baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Mengi Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema enzi za uhai wake, Mengi alikuwa mdau mkubwa kwao na alilipenda jeshi la polisi tofauti na matajiri wengine ambao wanakiona chombo hicho cha dola kama adui yao.

"Alikuwa anatushauri kwenye masuala ya usalama, ni mtu mwenye heshima kwa  watu wote. Alikuwa very hamble (mnyenyekevu) licha kuwa na fedha lakini alijishusha kwa watu.”

"Alikuwa mzalendo sana na jeshi hili. Najua siku ya kutoa heshima za mwisho watu watakuwa wengi, lakini nawahakikishia Watanzania polisi itaimarisha ulinzi ili mchakato huu uende vyema," amesema Sirro.

Kuhusu  taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii Sirro kuhusu kifo hicho, mkuu huyo wa jeshi la polisi nchini amesema polisi inafuatilia kwa karibu jambo hilo, lakini kwa sasa wanachokiangalia ni  kuhakikisha wanamaliza msiba huo kwa amani na utulivu.

"Polisi imeshafungua dokezo kufuatilia suala hili ili kujua ukweli maana yanasemwa semwa sana hata mimi nimeona leo asubuhi. Nawahakikisha Watanzania hatupuuzii taarifa hizi," amesema Sirro.