IGP Sirro atoa agizo kwa wapangishaji kuwa na picha za wanaowapangisha

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa akimuonyesha mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Simon Sirro Nyumba za askari zinazojengwa kutokana na michango iliyowashirikisha wadau.

Muktasari:

Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro ametembelea ujenzi wa nyumba za askari mkoani Morogoro na kutoa agizo kwa wapangishaji wa nyumba kuhakikisha wanakuwa na picha za wale wanaowapangisha

Morogoro. Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amewataka wapangishaji wa nyumba nchini kuhakikisha wanakuwa na picha za watu wanaowapangisha.

Pia, amewaonya askari wake kutopokea rushwa huku akiwasisitiza kutimiza wajibu wao kwa kutowaonea ria na kuwataka kutoa haki na kusimamia sheria.

IGP Sirro  ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 15,2019 wakati  akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa nyumba za askari zilizojengwa kutokana na michango iliyowashirikisha wadau mbalimbali.

Amesema wenye nyumba pale wanapo pangisha wateja wao na wanapoingia  mikataba nao ni vizuri wakawa na picha za wapangaji.

Amesema kumekuwepo na baadhi ya wapangaji kutumia mwanya huo katika kufanya uhalifu tunao ushahida katika nchi jirani na baadaye wakatokewa bila ya kufahamika .

Pia amesema ni vyema wananchi wakawa makini kwenye mitaa kwa kuhakikisha wanatambua watu wenye nia ovu na  kamati za ulinzi  za mitaa, vijiji, kata na tarafa kufanya kazi zao na wakiona kuna jambo si la kawaida ni vyema kupeana taarifa.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro ametoa Sh10 milioni zitakazosaidia hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba  kumi za askari wa Jeshi hilo, mkoani Morogoro ili ziweze kuanza kutumia ifikapo Mei 31, 2019.

"Napongeza kazi inayoendele na Mfuko wa IGP utatoa Shilingi 10 milioni  na wiki hii ( Ijumaa) zitakuwa zimeletwa  ziweze kusaidia  ukamilishaji," amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa nyumba za Polisi, Omary Abdallah Al – Saedy amesema ujenzi wa nyumba kumi umekamilika kwa asilimia kubwa na kilichobakia ni umaliziaji wa vifaa vya ndani kwa maana ya uwekeaji wa milango, na madirisha.

Amesema  nyumba hizo ni kwaajili  ya  kuishi familia mbili ambapo kila mmoja imegharimu kiasi kinachokaribia Sh25 milioni na  bado awamu ya pili itaendelea kufatana na michango itakayopatikana.