IGP Sirro atoa kauli kuzuiwa kwa mikutano ya wapinzani

Moshi/Dar. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amewataka viongozi wakuu wa vyama vya upinzani nchini, kuwasilisha malalamiko yanayohusu hujuma wanazodai kufanyiwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali kabla au wakati wa mikutano yao ya ndani ili aweze kuyashughulikia.

Kauli hiyo ya IGP Sirro imekuja wakati juzi Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alipoliambia Mwananchi kuwa licha ya Katiba ya Tanzania ya 1977 kuruhusu demokrasia ya vyama vingi, kuna uelekeo wa kuharamisha siasa za upinzani nchini kutokana na kamatakamata inayoendelea kwa viongozi wa vyama vya upinzani wanapofanya mikutano yao ya ndani.

Hata hivyo, IGP Sirro alisema jeshi hilo hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na halina upendeleo kwa baadhi ya vyama vya siasa, akisema tangu upinzani waanze kulalamika hawajawahi kupokea barua kuhusu malalamiko yao.

Lakini, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji alisema tayari walishaandika barua nyingi zinazohusiana na malalamiko ya kutotendewa haki na Jeshi la Polisi na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa, akiahidi kuwasilisha barua nyingine licha ya kuanzisha mbinu nyingine za kujijenga kisiasa badala ya mikutano hiyo ya ndani.

“Mwenye mamlaka ya suala la amani na utulivu katika nchi hii ni Jeshi la Polisi, kuona mikutano inamalizika salama ni kazi ya Polisi, mwenye mamlaka ya kuona kuna tatizo na kuweka pingamizi ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD),” Sirro aliliambia Mwananchi.

Alisema OCD anapokataa baada ya kuona kuna uvunjifu wa amani huwa anawaandikia barua (vyama), akitoa mapendekezo yake, lakini endapo chama hakijaridhika, kinaweza kukata rufaa ofisi ya IGP au kwa waziri mwenye dhamana.

“Kama kuna chama ambacho kinaona hakitendewi haki na Jeshi la Polisi, basi tuandikiwe malalamiko hayo ili tuweze kufuatilia kwa nini hiyo wilaya imeshindwa kutoa haki, waniandikie barua, nasisitiza sijawahi kupokea malalamiko yoyote ya barua kuhusiana na suala hilo (vikwazo vya polisi),” alisema Sirro.

Pia, alikanusha tuhuma za kuweka vikwazo kwa vyama vya upinzani akisema chombo hicho kimekuwa kikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Alipoulizwa ni mahali gani vyama vya upinzani vinakosea kwa sababu mikutano yao mingi ya ndani huzuiliwa huku ile ya CCM ikionekana kufanyika bila vikwazo, IGP Sirro alisema suala hilo lijadiliwe kwa takwimu zinazoonyesha ushahidi wa ukandamizaji kwa upinzani na upendeleo kwa mikutano ya CCM.

Wakati Sirro akihoji hayo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) lilikuwa likifanya mikutano yake ya ndani mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini ilisambaratishwa na polisi.

Jumamosi iliyopita, mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee alizuiwa kufanya mkutano wa ndani akiwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu na siku iliyofuata akiwa Bukoba mkoani Kagera, alikamatwa na polisi baada ya kumalizika kwa kikao chake cha ndani na kuwekwa rumande hadi alipoachiwa juzi.

Pia, mkutano wa Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche na wananchi wa jimbo hilo nao ulisambaratishwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita, huku polisi wakidai kuwa mbunge huyo aliandaa mkutano huo bila kupata kibali cha polisi.

Matukio hayo yamekuja siku chache tu baada ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kulitaka Jeshi la Polisi kutotumia nguvu kushughulikia migogoro ya kisiasa nchini.

Akiwa mkoani Manyara, Dk Bashiru alisema “tukianza kutumia mabavu katika kutatua migogoro yetu ni dalili za kushindwa kuongoza nchi, hakuna sababu wakati wananchi wanatii sheria bila shuruti.”

Kauli hiyo ilipongezwa sio na wasomi tu, pia na wananchi wa kawaida na hata makada wa CCM akiwamo Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliyesema, “Huyu ndiye Dk Bashiru ninayemfahamu.”

Alichokisema Mbowe

Akizungumza juzi na Mwananchi, Mbowe alisema vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji aliodai wanafanyiwa viongozi wa upinzani na polisi, haina tafsiri nyingine zaidi ya upendeleo kwa masilahi ya CCM.

“Haya mambo tutayasema mpaka lini? Tumeshasema sana na tumelalamika sana na tumeandika barua nyingi. Huo ni upendeleo ndiyo unasababisha wanatukamata.

“Wanatukamata, wanatuweka ndani na kutufunga. Suala la upinzani limekuwa ni criminality in Tanzania hii sio kwa Halima (Mdee) tu, mie nimekutana nayo.

“Huko tunafuatwa na polisi wenye silaha wanatuwekea kwa nguvu maaskari kanzu kwenye vikao vyetu. Ukandamizaji dhidi ya upinzani uko kwa kiwango kikubwa sana na dunia inaona.

“Kama alivyosema Rais Magufuli (John), Watanzania wa leo si wajinga, wanajua ku-analyze (kuchambua) mambo. Tumeamua acha tupambane na hali yetu, lakini haya yatafika mwisho,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alipozungumza na Mwananchi kwa simu juzi, alitaja mambo manne aliyodai kama yakizingatiwa, anaamini nchi itakuwa salama.

Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Vunjo alisema mambo yoyote ya maendeleo nchini yanatakiwa yazingatie mambo manne.

“Ili nchi iwe salama, maendeleo yoyote yawe ni ya kisiasa au kiuchumi na kijamii, lazima yazingatie mambo manne ambayo ni utu, utulivu wa fikra, muda na thamani ya pesa inakuwa ya mwisho.

“Uhuru na haki zile za msingi zinazopatikana katika Katiba yetu (ya 1977) ndiyo chimbuko la maendeleo endelevu. Ukikiuka moja tu mathalani la utu, lazima ilete shida,” alisisitiza Mbatia.

“Kama kila utawala unakuja na mambo yake mapya tutakuwa tunapiga danadana. Na hili naliongea kama mwenyekiti wa TCD. Vyama vyote ni lazima tuheshimu katiba na tusibaguane kwa itikadi,” alisema mwenyekiti huyo.

Mbatia alisema vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa vina haki sawa ya kufanya siasa na si sahihi kwa Jeshi la Polisi kuona mikutano ya CCM ni halali, lakini mikutano ya ndani ya upinzani ni haramu.

“Tusipozingatia hayo mambo na kuheshimu Katiba ya nchi na sheria zetu, tutasababisha chuki na visasi. Nayasema haya kwa nia njema kabisa ya kulitakia amani Taifa langu mama la Tanzania,” alisema.

Madai ya viongozi hao yamekuja wakati Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akisema ofisi yake haijawahi kupokea malalamiko ya maandishi ya vyama kuzuiwa kufanya mikutano.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alikaririwa na gazeti hili akithibitisha kauli hiyo ya Jaji Mutungi kuwa ni kweli chama chake hakijawahi kufanya hivyo akisema hilo liko juu ya uwezo wake.