UCHOKOZI WA EDO: Inawezekana na ‘kibarua’ cha Profesa kimeisha

Baada ya yule mzee kuondoka kundini nahisi kama vile kibarua cha Professa kitakuwa kimekoma. Kazi yake ingeweza kuendelea kama yule bwana angeng’ang’nia kubakia chamani, lakini sasa ameachwa peke yake na hana mshindani.

Profesa atafanya nini zaidi? Hatuwezi kujua. Mwisho umefika. Wale waliokuwa wanashutumu kwamba Profesa alikuwa analipwa kwa yote aliyokuwa akiyafanya labda huu ni wakati wa kutuambia kwamba huenda kuna ‘ajira’ nyingine atapewa.

‘Waajiri’ wake kwa yote aliyokuwa akiyafanya tunadhani hawatakuwa na sababu za kumlipa. Mambo yangekuwa matamu zaidi kama yule bwana aliyeachia ngazi angeamua kubaki madarakani hapo kibarua kingeendelea, lakini sasa jicho la mwewe linaona mambo huenda yasiwe mazuri kwa Professa.

Wakati mwingine huu ndio ubaya wa hizi kazi. Ukiangalia karibu, wagomvi wako wanaangalia mbali zaidi na kuhitimisha kibarua chako. Ni wazi kwamba yule bwana alikuwa amejipanga kuondoka siku nyingi. Alikuwa anasubiri ‘pilato’ ahalalishe madhabahuni. Ilipofanyika hivyo alitoka ofisi za pilato akaenda jumba lingine. Hakwenda ofisi nyingine za pilato kwa ajili ya kukata rufaa. Alijua angekuwa anacheza mchezo wa kitoto.

Hatimaye amehama timu yake na kwenda nyumba ya jirani bila ya matarajio ya wale waliokuwa wanachezesha mchezo. Sasa anahama na mashabiki wake ambao kwa muda mrefu wamekuwa waaminifu kwake.

Karata ya mwisho ambayo inaweza kumpatia ajira Professa ni kipute cha mwakani 2020. Naanza kupata hamu tu ya kujua jinsi ambavyo atashiriki katika kipute hicho. Atacheza nafasi gani uwanjani? Kiungo mkabaji dhidi ya wenzake au kiungo mshambuliaji kwa ajili ya kushambulia?

Chama chake kitajaribu kumuondoa Namba Moja katika nafasi yake? Wanaweza kucheza mchezo wa kuigiza wa kujifanya wanataka kumuondoa Namba Moja madarakani, lakini sidhani kama filamu itakuwa nzuri. Haitauza sokoni.

Yawezekana wakaigiza huku wakifanya kazi ya kukwaruzana na wenzao kwa umaridadi mkubwa. Wenzao wakienda kushoto, wao wanaenda kulia. Wenzao wakinuna, wao wanatabasamu. Wenzao wakisema ‘hili hatutambui’, wao watasema ‘hili tunalitambua’. Nadhani hii ndio kazi ambayo inaweza kubakia kwa Bwana Profesa.