Iran yatungua ndege ya Marekani

Muktasari:

Marekani imekiri taifa hilo kutungua ndege yake hata hivyo, imekanusha taarifa kwamba waliingilia anga yao


Iran. Jeshi la Iran limetungua ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk, kusini mwa Jimbo la Hormozgan.

Kwa mujibu wa jeshi hilo la Iran, ndege hiyo ya Marekani imekiuka kanuni za anga za Iran karibu na mlango bahari wa Hormuz.

Shirika la habari la Al Jazeera limesema kuwa Marekani imekiri taifa hilo kutungua ndege yake hata hivyo, imekanusha taarifa kwamba waliingilia anga yao.

Maafisa wa Marekani wamedai kuwa ndege yake ilikuwa katika anga la kimataifa ilipokuwa kwenye anga ya kimataifa kwenye eneo la mpaka kati ya ghuba ya Oman na Uajemi.

Tukio hilo limetokea siku kadhaa baada ya wizara ya ulinzi ya Marekani kusema kuwa watapeleka vikosi 1,000 zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana na mvutano kati ya mataifa hayo mawili.

Katika mgogoro huo, Marekani iliishutumu Iran kushambulia kwa mabomu meli za mafuta katika Ghuba ya Oman.

Mzozo huo ulishika kasi siku ya Jumatatu wakati Iran iliposema kuwa itazidisha kiwango cha urutubishaji wa madini ya Urani kinyume cha makubaliano na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2015. Iran imefikia uamuzi huo baada ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani.