JPM atoa maagizo ajali iliyoua 19 Songwe, ndugu wasimulia kauli za mwisho

Mbozi. Vilio, majonzi na simanzi jana vilitawala katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Mkoa wa Songwe wakati ndugu walipofika kutambua miili ya wapendwa wao 19 waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea juzi usiku.

Baadhi walieleza jinsi walivyozungumza na ndugu zao saa chache kabla hawajapata ajali huku Rais John Magufuli akituma salamu za rambirambi na kuzitaka mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

Watu hao walifariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea katika mteremko wa Mlima Senjele, Songwe baada ya lori lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Mbeya kuligonga basi la abiria kwa nyuma.

Basi hilo baada ya kugongwa, liliingia katikati ya lori jingine lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo hivyo.

Yusta Mwakatale, ambaye dada yake Menistar alifariki katika ajali hiyo alisema aliondoka nyumbani akiaga anakwenda kumchukua mama yao anayeishi Mbeya.

“Sikujua kama kipenzi changu na rafiki yangu ndiyo ananiaga vinginevyo asingeenda katika safari hiyo ili ayanusuru maisha yake,” alisema Yusta.

Robert Mwakilemile, aliyempoteza baba yake katika ajali hiyo alisema alikuwa akienda kuitembelea familia yake lakini alifikwa na mauti kabla ya kufika alikokuwa anakwenda.

“Baba aliwasiliana na mama alipofika mji mdogo wa Mlowo. Ilikuwa saa mbili usiku, ilipofika saa tatu usiku mama aliendelea kumpigia simu ikawa haipatikani mpaka tulipopata taarifa ya ajali,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori kufeli breki likiwa katika mwendo kasi kwenye mteremko huo na kuyagonga magari mawili kwa nyuma.

Akizungumza hospitalini hapo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela alimuagiza Kamanda Kyando kuhakikisha magari yanapita kwa zamu katika eneo hilo ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Salamu za rambirambi

Rais Magufuli jana alituma salamu za rambirambi na kumtaka mkuu wa mkoa kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.