JWTZ latoa onyo wanaovamia mapori, mipaka

Muktasari:

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema imejipanga kupambana na  wahalifu wanaotumia mapori kufanya uhalifu katika mpaka wa magharibi.

Kibondo. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema litakula sahani moja na watu wanajificha katika mapori na kufanya vitendo vya kiuhalifu katika mpaka wa magharibi.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya matukio ya kiuhalifu kukithiri katika wilaya ya Kasulu, Kibondo mkoani Kagera nchini Tanzania kwa kuteka watu,  kuporwa mali zao pamoja na kuchapwa viboko.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Agosti 12,2019 wakati wa kuahirisha shughuli ya utayari la kijeshi lililopewa jina la KIKAKA, lililofanyika wilayani Kibondo, Mkuu wa Brigedi ya Magharibi, Brigedia Jacob Mkunda amesema jeshi limejipanga kupambana na uhalifu na kwamba wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano pale unapohitaji.

Amesema jeshi hilo lita hakikisha linalinda amani na usalama wa wananchi wake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika mipaka.

"Zoezi hili litakuwa endelevu na hatutakubali kuona misitu na mapori yanavamiwa na raia kutoka nchi za jirani na kutumia kufanya uhalifu na kutishia usalama wa wananchi wa mkoa wa Kigoma," amesema.

Amesema suala la ulinzi na usalama sio la jeshi pekee bali kila taasisi pamoja na wananchi wanatakiwa kuwafichua watu wote wanaoingia  nchini bila vibali na kufanya uhalifu pamoja na raia wanaoshirikiana nao katika vitendo hivyo.

Mkuu wa mafunzo  na utendaji  kivita Kanali, Wilson Ibuge amesema mapori yote yaliyopo katika mipaka ya magharibi ni mali ya jeshi hilo na kwamba ndio eneo lao la kazi na kwa sasa ndiyo wameanza kazi rasmi katika mapori hayo.

"Zoezi hilo ni endelevu na linapeleka salamu kwa wavamizi wa maeneo hayo na wakitaka usalama wao ni kuacha kujihusisha na mambo ya kijangili na uhalifu pamoja na wananchi wa Tanzania wanaoshirikiana na wahalifu  watashughulikiwa.

Kamanda wa kikosi cha 24 KJ, Meja Jonson Luhovya amesema ndani ya siku 13 ya zoezi hilo askari walifanya mazoezi katika maeneo mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo Mvugwe, Malagarasi, Kagerankanda, Busunzu, Nyarugusu na Kisogo pamoja na maeneo yanayo karibia kambi ya Kanembwa.

Amesema zoezi hilo liliweza kubaini baadhi ya raia kutoka nchi jirani ya  Burundi, kuwepo katika eneo la mapori hayo wanaojihusisha na uvunaji wa mihogo baada ya hapo wanajihusisha na mambo mengine ya ikiwepo uhalifu.

Amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mafuta na kwamba endapo wakipata lita 300 kila mwezi za kupiga doria katika mapori hayo itasaidia mapori hayo kuwa salama.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga, Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Simon Annange amesema eneo kubwa la pori hilo ni chanzo cha  mto Maragalasi linalomwaga maji katika ziwa Tanganyika ni lazima lilindwe kwani wasipofanya hivyo litasababisha kuongezeka kwa joto ziwani na kusababisha samaki kukimbia.

Zoezi hilo linalengo la kujifunza namna ya kukabiliana na maadui, kuainisha matumizi ya silaha  za kivita, kufanya tathmini ya utendaji kazi wa silaha za kikosi, kuimarisha utendaji kazi wa kikosi, kuwezesha  maofisi   kujua  matumizi ya silaha  za kivita katika nyakati zote na kuwajengea uwezo maafisa wa kutoa amri na matumizi ya redio nyakati za vita.