Jafo atoa agizo kwa halmashauri zote Tanzania

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jaffo akizungumza na mshauri wa huduma za mipango miji kutoka Benki ya dunia, mhandisi Mussa Natty (kushoto). Katikati ni mtaalamu wa mipango miji kutoka Benki ya dunia, MaryGrace Lugakingira na kulia ni mkuu wa wilaya Kigoma, Samson Anga. Picha na Anthony Kayanda.

Muktasari:

  • Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo ameagiza halmashauri zote nchini kuzingatia maslahi ya umma katika upangaji wa matumizi ya fedha inayotokana na makusanyo ya ndani

Kigoma. Serikali imeagiza halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele katika miradi ya maendeleo badala ya kutumia fedha ya makusanyo ya ndani kwa matumizi yasiyo na tija kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Machi 15, 2019 mjini Kigoma wakati wa uzinduzi wa kazi ya kuunganisha mfumo wa kukusanya mapato (LGRCIS) na mfumo wa taarifa ya kijiografia (GIS) katika miji inayotekeleza mradi wa kuboresha manispaa na majiji nchini (TSCP).

Amesema baadhi ya halmashauri zinakusanya fedha kutoka vyanzo vya ndani lakini nyingi zinatumika katika matumizi yasiyo na tija kwa wananchi.

"Nilikuwa nasoma taarifa ya robo mwaka kutoka halmashauri ya wilaya Songea (Songea vijijini) inayoonyesha walikusanya Sh76 milioni, wakatumia Sh24 milioni kutengeneza gari la DED (mkurugenzi wa halmashauri), Sh15 milioni zikatumika kwa safari na miradi ya maendeleo wakapeleka Sh7 milioni," amesema Jafo.

"Ni aibu kuona Sh7 milioni ndizo zinazopelekwa kujibu shida za wananchi kati ya makusanyo ya Sh76 milioni, lazima fedha ya kutosha itengwe kutatua changamoto za wananchi wetu," amesema Jaffo.

Ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini wahakikishe wanadhibiti matumizi ya fedha kwenye halmashauri zao ili fedha inayokusanywa ikatumike kutatua kero za wananchi.

"Inawezekana tatizo hili lipo hata hapa Kigoma Ujiji, lazima madiwani na watendaji muwe na mtazamo wa kuwatumikia wananchi," amesema.

Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Samson Anga amesema wakuu wa wilaya watasimamia kazi hiyo vizuri ili fedha inayokusanywa ilete tija kwa jamii.

"Waziri acha tufanye kazi, nakuomba ukisikia maneno yoyote uyapuuze, sasa tunaingia kazini ili kuhakikisha mapato ya halmashauri yanapanda," alisisitiza Anga.

Waziri Jafo alikuwa na ziara ya siku mbili mkoani Kigoma iliyoanza jana Alhamisi na kumalizika leo Ijumaa.