Jafo atoa maagizo sita mabasi mwendo kasi

Saturday March 16 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Adha ya usafiri wanaopata watumiaji wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam umemfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kutoa maagizo sita akitaka yatekelezwe ili mradi huo utoe huduma kwa ufanisi badala ya kusuasua.

Kwa siku kadhaa, abiria wanaotumia usafiri huo wamekumbana na changamoto ya kukaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na uhaba wa mabasi hayo hali iliyosababisha baadhi yao kuchelewa katika shughuli zao mbalimbali.

Abiria hao waliozungumza na Mwananchi, wamesema wanalazimika kukaa kituoni saa moja au saa moja na nusu wakisubiria usafiri huo kwenda maeneo mbalimbali ya kazi.

Wengine walikwenda mbali zaidi wakitaka safari zinazofanywa na mabasi hayo kutoka Kimara hadi Mbezi zifutwe kwa kuwa hakuna mabasi ya kutosha ya mradi huo yanayoanzia Kimara kwenda katikati ya jiji.

Siyo hao tu bali wengine waliiomba Serikali kuweka sanduku maalumu ili watu wapige kura ya kutaka mradi huo uendelee au atafutwe mwekezaji mwingine atakayeusimamia kwa ufanisi.

Na kilio cha watumiaji wa usafiri huo kikasikika. Jana Waziri Jafo alitembelea kituo cha mwendokasi cha Kivukoni kisha kuwaambia wanahabari, “Siridhishwi wala kufurahishwa na hali ya kusuasua kwa usafiri huu unaotegemewa kwa kiasi kikubwa na wananchi wengi.”

“Kuna matatizo yanayojitokeza mara kwa mara na kuleta usumbufu kwa wananchi, lakini sijaona njia stahiki ya kuridhisha zilizochukuliwa kwa watoa huduma ili kupata ufumbuzi. Matatizo haya yanajitokeza kwenye vituo vya Kimara- Kivukoni na Gerezani nyakati za asubuhi na jioni,” alisema Jafo.

Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa mabasi, lakini kuna wakati magari hayo yameonekana yakisafiri yakiwa hayana abiria au yameegeshwa pembeni ya vituo wakati wananchi wamejazana vituoni kuyasubiri.

Baada ya maelezo hayo, Jafo alitoa maagizo sita kwa kumuelekeza mtendaji mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Leonard Lwakatare ahakikishe anaongeza mabasi 10 ya ‘Feeder Road’ maarufu ‘Bombadier’yanayobeba abiria kutoka Mbezi hadi Kimara yahamishiwe barabara ya mwendokasi .

Alisema mabasi hayo yatagawanywa matano, yatakwenda njia ya Gerezani na mengine Kivukoni ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mabasi hayo.

“Mabasi haya hayataruhusiwa kubeba abiria katika vituo vya mwendokasi vya kawaida kutokana na namna milango ilivyotengenezwa. Hivyo yatachukua abiria kuanzia mwanzo wa kituo na kuwashusha mwisho wa kituo asubuhi na jioni,” alisema

Agizo la pili aliitaka Dart kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kuangalia namna ya kuongeza mabasi ya kawaida yatakayokuwa yakichukua abiria watakaoshuka Kimara wakitokea katikati ya jiji na wale watakaokuwa wakitokea Mbezi kwenda Kimara.

“Agizo la tatu Dart ihakikishe Udart ambayo ina dhamana ya kusafirisha abiria inafanya matengenezo ya mara kwa mara ya mabasi yake ili kuondoa usumbufu unaojitokeza wa upungufu wa magari,” alisema Jafo.

Advertisement