Jaguar atoa kauli nyingine kuhusu Watanzania kuondoka Kenya ndani ya saa 24

Muktasari:

Video iliyosambaa ikimuonyesha Jaguar akitoa matamshi ya kuwataka Watanzania na raia wengine wasio Wakenya kuondoka nchini humo ndani ya masaa 24 imekuwa gumzo hali iliyosababisha kiongozi huyo kutolea ufafanuzi wa alichokisema

Baada ya kusambaa kwa video inayomuonyesha mbunge wa Starehe nchini Kenya Charles Njagua maarufu Jaguar akiwataka Watanzania na Waganda wanaofanya biashara zao nchini Kenya kuondoka ndani ya masaa 24 la sivyo watawatoa kwa nguvu, hatimaye kiongozi huyo ambaye pia ni mwanamuziki ametolea ufafanuzi kuhusu kauli yake.

Akitumia ukurasa wake wa Twitter leo Jumanne Juni 25, 2019 kiongozi huyo amesema kauli hiyo iliwalenga Wachina ambao wamevamia masoko ya Wakenya na kuendesha biashara zao zinazoweza kufanywa na wananchi wa Kenya na kauli yake hiyo  haikuwalenga watu wengine

Katika ukurasa wake wa Twitter anaotumia jina la @RealJaguarKenya ameandika “My sentiments echoed yesterday with a directive to C.S Matiang’i was meant for the Chinese who have invaded our markets making businesses almost unbearable bearing for our citizens. I am not against any regional unions that are meant to promote both local and regional trade”

Kauli ya kiongozi huyo imekuwa gumzo mitandaoni huku Watanzania mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusu video iliyosambaa ambayo wengi wanadai inaleta ubaguzi pamoja na kuzua hofu kwa raia wa Tanzania wanaoishi na kufanya biashara zao nchini Kenya

Hata hivyo nchini Tanzania Tayari Spika wa Bunge Job Ndugai amemtaka Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa leo jioni Jumanne Juni 25,2019 kutoa kauli ya Serikali kuhusu utata huo unaoendelea.