Jaji Warioba azungumzia Rasimu ya Katiba, wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Jaji Warioba azungumzia Rasimu ya Katiba

Muktasari:

Wakati mjadala kuhusu uhalali wa wakurugenzi kusimamia au kutosimamia chaguzi nchini ukishika kasi mitandaoni, mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema maoni ya wananchi kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba yaliweka wazi namna gani wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi wangepatikana

 


Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu uhalali wa wakurugenzi kusimamia au kutosimamia chaguzi nchini ukishika kasi mitandaoni, mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema maoni ya wananchi kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba yaliweka wazi namna gani wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi wangepatikana.

Warioba alitakiwa kutoa maoni yake kuhusu uhalali wa wakurugenzi kutosimamia au kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia msingi wa maoni ya wananchi katika rasimu hiyo hususani eneo la tume huru.

Mjadala huo ulishika kasi ikiwa ni siku chache baada ya Serikali kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia Wakurugenzi  kusimamia chaguzi.

“Kwenye rasimu imezungumzia ni kwa vipi wajumbe wa tume watapatikana, hayo mengine unayosema hayamo katika rasimu,” amesema Jaji Warioba huku akifafanua kuhusu maoni ya wananchi ndani ya rasimu hiyo.

“Tunajua ni maoni yao (wananchi) ,tunasema waendelee kutoa maoni, sisi hatuingilii , hatutaki kuingilia malumbano ya kisiasa wakati huu, wanaweza kulizungumza tu ila sisi hatutaki kuhusishwa.”

Sehemu ya Pili ya rasimu hiyo Ibara ya 190, inaelezea sifa za kupatikana kwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume hiyo huku ikiwataja wabunge, madiwani na watumishi wa umma kutokuwa na sifa za kuwa wajumbe wa tume hiyo. 

Katika ibara ya 191, inasema kutakuwa na Kamati ya uteuzi wa mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo itakayoundwa na majaji wakuu watatu na maspika watatu kutoka Tanganyika, Zanzibar na Januhuri ya Muungano pamoja na mwenyekiti wa tume ya maadili ya uongozi na uwajibikaji.

Alipoulizwa nini mtazamo wake baada ya serikali kukata rufaa katika hukumu ya Mahakama Kuu, Jaji Warioba alisema: “Nimesema sisi katika mazungumzo haya hatumo.”