Jaji alivyotupilia mbali shauri la Zitto kupinga muswada wa Vyama vya Siasa

Monday January 14 2019

Kiongozi wa Act wazalendo, Zitto Kabwe,

Kiongozi wa Act wazalendo, Zitto Kabwe, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusino wa Umma wa Cuf Taifa, Salim Bimani(wa pili kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Cuf, Joram Bashange (wa pili kulia) wakimsikiliza wakili Jeremia Mtobesya walipokuwa katika chumba cha Mahakama kuu jijini Dar es Salaam leo, wakisubiri kusikilizwa kwa uamuzi wa shauri la kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa. Kulia ni kiongozi wa jopo la mawakili upande wa walalamikaji, Mpare Mpoki. Picha na Ericky Boniphace 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Tanzania imetupilia mbali shauri la Kikatiba la kupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, lililokuwa limefunguliwa na wanasiasa watatu kwa niaba ya vyama 10 vya upinzani.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Januari 14, 2019 na Jaji Benhajj Masoud, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la Serikali, kuwa shauri hilo halikuwa halali kuwepo mahakamani kwa kuwa lilikiuka utaratibu na sheria.

Shauri hilo la Kikatiba namba 31 la mwaka 2018 lilifunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu na wanasiasa watatu akiwemo Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, kwa niaba ya muungano wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Wengine ni kaimu katibu mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Joran Bashange na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano CUF, Salim Bimani wote kutoka kambi ya Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad.

Wanasiasa hao walikuwa wakipinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada kupingwa mahakamani.

Pia walikuwa wakipinga muswada huo wakidai unakiuka haki za Kikatiba za kisiasa kwani unazifanya shughuli mbalimbali za kisiasa kuwa jinai na unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo  yakiwemo ya uongozi.

Serikali iliweka pingamizi ikiiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali, huku ikiwasilisha jumla ya hoja kumi.

Hata hivyo, Jaji Masoud katika uamuzi wake wa kutupilia mbali shauri hilo amezingatia hoja mbili tu kati ya hizo kumi, ambazo zimetosha kulitupilia mbali.

Hoja hizo za pingamizi la Serikali ambazo Jaji Masoud amezizingatia ni pamoja na hoja ya tatu ya pingamizi la Serikali kuchanganya maombi mawili katika shauri moja na sehemu ya hoja ya nane kwamba shauri hilo linakiuka sheria.

Jaji Masoud amesema walalamikaji hawakupaswa kuomba Mahakama itamke kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu kinakiuka Katiba wakati huohuo wanaomba pia mahakama itamke kuwa muswada huo unakiuka katiba.

Amesema maombi hayo mawili yanategemeana, kwani ombi la pili la muswada linategemea uamuzi wa ombi la kwanza la kupinga kifungu hicho cha sheria na kwamba walipaswa kwanza wafungue shauri katika ombi la kwanza na kama wangekubaliwa ndipo wangefungua shauri la kupinga muswada. 

Katika hoja nyingine Jaji Masoud amesema kwamba shauri hilo linakiuka kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu, kwani hawakufuata utaratibu unaoelekezwa katika kifungu hicho.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu yeyote anayedai haki zake zinakiuka au zinaelekea kukiukwa anapaswa kutafuta nafuu kwa kutumia njia nyingine zilizopo kwanza kabla ya kwenda mahakamani.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo lilidai kuwa walalamikaji hawakukidhi matakwa ya kifungu hicho kwani hawakutumia njia nyinginezo zilizopo kabla ya kukimbilia mahakamani.

Walibainisha kwamba mlalamikaji wa kwanza, Zitto ni mbunge tena mzoefu ambaye anazijua Kanuni za Bunge zikiwemo za mwaka 2016 ambazo zinampa nafasi kushiriki kujadili muswada wowote na kutoa maoni na mapendekezo yake kwa uhuru na zinampa kinga.

Walidai kuwa pia kanuni hizo zinampa mamlaka ya kumuomba Spika aisimamishe kwa muda maalum upitishwaji wa muswaada huo ili kumpa nafasi kuwasilisha maoni yake.

Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa hata hivyo walalamikaji hao hawakutumia njia hizo badala yake wamekimbilia mahakamani moja kwa moja, kinyume na masharti ya kifungu hicho.

Akizungumzia uamuzi huo, Zitto amesema kuwa wanaheshimu uamuzi wa Mahakama lakini akasema kuwa wataendelea na mapambano ya kile alichokiita kudai haki kwa kutumia njia hiyo hiyo ya Mahakama.

Advertisement