Jalada la mume, mke wenye kesi ya dawa za kulevya lipo kwa DPP

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Ayub Mfaume Kiboko na mkewe, Pilly Mohamed Kiboko umedai kuwa jalada lipo kwa DPP.

Dar es salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Ayub Mfaume Kiboko na mkewe, Pilly Mohamed Kiboko umedai kuwa jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.

Kiboko na mkewe wanakabiliwa na shtaka moja katika kesi ya uhujumu uchumi namba 29/2018, ambapo wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas amedai leo Jumatatu Aprili 15, 2019 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na jalada lipo kwa DPP kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi.

Baada ya uamuzi huo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema shauri hilo lipo mahakamani hapo miezi kumi sasa na matarajio ni kwamba kesi hiyo itakapokuja tena upande wa mashtaka utakuja na lugha nyingine.

"Kila siku mkija hapa mnasema jalada lipo kwa DPP sasa ni miezi 10 imeshapita, tunachotaka mfuatilie ili kujua imefikia wapi," amesema Simba.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 29, 2019 itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wataendelea kukaa rumande.

Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 251.25.