Jina la Halima Mdee lafuta hotuba nzima ya upinzani bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwa amekishika kitabu cha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambacho kina maoni ya kambi hiyo  kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya  Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo alizuia kusomwa bungeni kwa madai kimejaa makosa. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Bunge la Tanzania limeifuta hotuba ya upinzani kuhusu wizara ya fedha na mipango kwa maelezo imejaa makosa mengi ikiwemo kuandikwa juu jina la mbunge aliyesimamishwa kuonyesha kuwa alishiriki

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amezuia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kusoma maoni yao  kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa madai imejaa makosa.

Ametoa zuio hilo bungeni leo Jumatatu Juni 3, 2019, Spika Ndugai amesema sababu mojawapo ni jina la mbunge wa Kawe (Chadema) Halima ambaye ametajwa kwenye kitabu cha hotuba hiyo ukurasa wa mbele.

Amesema hotuba nzima kuanzia ukurasa wa kwanza hadi mwisho imejaa maneno yasiyo faa wakati wanajua maandishi hayo yatadumu hata miaka 100 ijayo.

Msemaji wa upinzani wa Wizara ya Fedha Halima Mdee amesimamishwa na Bunge kuhudhuria mikutano mwili ya Bunge kuanzia huu unaoendelea wa 15 wa Bunge la Bajeti kwa kosa la kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwamba Bunge ni dhaifu.

"Hapa tunatoka sisi lakini kuna vizazi vyetu na wajuu na vitukuu wetu watasoma vitabu hivi, haiwezekani mtu umesimamishwa halafu unashiriki kufanya kazi za Bunge," amesema Ndugai.

Hivi karibu Ndugai aliwaambia wapinzani bungeni kuwa hotuba zao zitaruhusiwa kusomwa isipokuwa aliwatahadharisha kuwa makini na uandishi usioleta mgongano.

Hotuba hiyo iliyozuiwa ilikuwa isomwe na Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde ambaye ni Naibu Waziri kivuli katika Wizara ya fedha na ndiye aliyesoma hotuba hizo kwa miaka miwili kutokana na Mdee kuwa nje kwa adhabu mbalimbali.