RIPOTI MAALUMU: Jinsi bidhaa zilizotupwa dampo zinavyorudishwa sokoni Dar es Salaam-2

Wednesday January 16 2019

 

Awali, mwandishi wetu alikutana na mmoja wa wazoa taka, Matatizo Athanas (siyo jina lake halisi) ambaye pia anauza vitu vinavyookotwa dampo.

Alisema wao ni mawakala tu wa kuuza bidhaa hizo huku akiutaja mtandao wa vinara wa biashara hiyo.

“Ukitaka kuuza bidhaa yako kwa urahisi tengeneza uhusiano na hao niliokutajia wao ndio wanaweza kukusaidia kupata soko kwasababu wana mabosi wao wanaowatuma kutafuta hizo bidhaa huku dampo,” alisema Matatizo.

“Si rahisi kukuonyesha mabosi wao maana wana usiri mkubwa labda mpaka wakuamini.”

Matatizo alimwonyesha mwandishi boksi lililojaa sabuni, dawa za meno, majani ya chai ya Fahari kutoka Kenya ambapo bidhaa zote zilikuwa zimepita muda wa matumizi tangu Desemba, 2016.

Pia alimwonyesha maziwa ya unga aina ya Nestle yaliyokwisha matumizi tangu Februari 2018 huku akieleza kuwa uuzaji wa bidhaa hizo ndiyo kazi inayomweka mjini.

Akiwa ameongozana na mwandishi wetu, Matatizo alikuwa amebeba sabuni za kuogea aina ya Ayu na dawa za meno ambavyo vyote alikuwa amevijaza kwenye begi la mgongoni akienda kumuuzia mmoja wa mawakala.

Baada ya kutengeneza mazingira ya kuingia kwenye dampo la Kinyamwezi kwa kumtumia Matatizo, mwandishi alipata fununu kuwa makontena tisa ya saruji iliyokwisha muda wake kutoka Pakistan itamwagwa damponi.

Alibahatika kushuhudia makontena mawili yenye urefu wa kati ya futi nane mpaka 10 yakiwa kwenye malori (namba zake tunadhifadhi) yakiingia ndani ya dampo majira ya saa sita mchana. Hiyo ilikuwa Novemba 6, mwaka jana.

Makontena hayo yaliyokuwa yakisindikizwa na gari ndogo (tunazo namba zake, mali ya shirika la umma) yalikuwa yamejazwa saruji aina ya Tiger na ilidaiwa kwamba yalitokea katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wao, madalali na wanunuzi wa bidhaa hizo (majina tunayahifadhi) walikuwa mstari wa mbele kusimamia kazi hiyo huku wengine wakipakua saruji hiyo kutoka ndani ya makontena kabla ya kufukiwa ardhini, huku nyingine ikifichwa vichakani.

Upakuaji huo uliodumu kwa zaidi ya saa moja na nusu, ulisimamiwa na dada mmoja na muda mfupi baada ya magari yaliyoleta makontena kuondoka, bodaboda zilianza kumiminika eneo hilo na kuanza kupakia mifuko ya saruji iliyokuwa imefichwa kwenye vichaka.

Siku iliyofuata saruji nyingi iliyotupwa ilikuwa imefungiwa kwenye vibanda na nyumba zilizopo dampo, huku mmoja wa wauzaji akimweleza mwandishi wetu aliyejifanya kuwa mnunuzi kuwa ana mifuko 18 ndani.

“Hapa nimebakiza mifuko 18, nahitaji mtu atakayechukua yote na si rejareja, tunavyoongea kuna mteja ambaye anahitaji kwa bei ya Sh10,000 kila mfuko amepatikana,” alisema muuzaji huyo.

Alipoulizwa kama wanajua saruji nyingi iliyomwagwa siku iliyopita imeishia mikononi mwa watu, mmoja wa maofisa upelelezi katika kituo cha polisi kilichopo eneo hilo, alisema hajui lolote.

Hata hivyo alisema kuwa anazo taarifa kutoka bandarini kuwa kuna makontena mengi ya saruji ambayo inatakiwa kuteketezwa dampo, lakini anashangaa kupata fununu kuwa inauzwa mitaani.

Licha ya ofisa huyo kudai kuwa kuna makontena mengi ya saruji iliyopaswa kuteketezwa, Mwananchi lilishuhudia makontena sita yaliyofikishwa dampo. Makontena mawili ya kwanza yalifikishwa Novemba 4, mawili Novemba 6 saa saba mchana huku mawili ya mwisho yakifikishwa saa 12 jioni.

Chokoleti, pipi

Wiki moja baada ya kumwagwa saruji, yaliletwa makontena manne ya biskuti, pipi, chokoleti, korosho, mazulia na kanzu vilivyomwagwa Alhamisi na Ijumaa ya Novemba 15 na 16. Licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali, bidhaa hizo zilichukuliwa na wajanja na kurudishwa mitaani.

“Baada ya kumwagwa tu usiku watu tuliingia kazini tukafukua, yale mazulia yaligombaniwa ‘kinoma’ hata polisi waliokuja kuyatupa na wao walichukua na mpaka risasi zilipigwa jana,” alisema mmoja wa mawakala wa biashara hiyo.

Madalali, wanunuzi bidhaa

Madalali na wanunuzi wa bidhaa katika dampo hilo wana ratiba kamili ya bidhaa zinazoingizwa na kumwagwa au kuteketezwa.

Mmoja wa mawakala (jina tunalihifadhi), anasema wateja wao wengi wapo Kariakoo.

Anasema ili kupata bidhaa za dampo mtu anatakiwa kuwa mjanja na pia amiliki ghala la kuhifadhia kabla ya kutafuta soko mbali na dampo hilo.

Pia, anasema bidhaa zinapofikishwa kumwagwa huwa wanavizia muda ambao wamwagaji wanaodoka au usiku wa manane ndipo wanajitosa kuanza kufukua.

“Kuna bidhaa zingine huwa zinafukiwa (ardhini), tunachofanya ni kufukua kwa kutumia majembe na mikono,” anasema wakala huyo.

Mihuri inavyopigwa

Katika dampo hilo kuna watu maalumu ambao wanapiga mihuri kuongeza muda wa matumizi ya bidhaa hizo, ambapo zinazopigwa muhuri huuzwa kwa haraka zaidi.

“Tulikuwa na katoni 100 za maziwa ya unga, tuliwatafuta wataalamu wakatupigia muhuri upya tukawalipa Sh300,000, tukauza maziwa, tukapata kama Sh4 milioni,” anasema mmoja wa mawakala wa bidhaa hizo.

Siku nyingine, bila yeye kujua, Mwananchi lilimuomba wakala huyo alitafutie bidhaa za aina yoyote zinazofikishwa dampo kuteketezwa, ambapo aliahidi kufanya hivyo kwa malipo.

Novemba 29, wakala huyo alimwandikia mwandishi wetu ujumbe mfupi wa maandishi akimweleza kuwasili kwa nguo za mitumba damponi hapo na Desemba Mosi alituma ujumbe mwingine akimtaarifu kuna kuna ‘lotion’ na ‘cream’ (vipodozi), sabuni, mafuta ya nywele na dawa za nywele.

Alisema zipo zaidi ya katoni 10 amezihifadhi kwa ajili ya kumuuzia.

Bidhaa zinavyouzwa

Mara nyingi bidhaa na vyakula vinavyomwagwa katika dampo la Kinyamwezi huuzwa mitaani kwa bei rahisi. Ndani ya dampo vitu hivyo huuzwa kwa bei ya karibu na bure.

Kwa mfano, ndani ya dampo hilo kiroba cha kilo 25 cha ngano au mchele huuzwa hadi Sh5,000 na bei hubadilika unapotoka nje ya dampo na kutegemeana na mahali unapopelekwa.

Vilevile ndani ya dampo hilo kopo moja la maziwa huuzwa hadi Sh1,000 na likitolewa nje bei yake inafika hadi Sh2,500.

Mwisho

Advertisement