Jinsi wabunge walivyohoji vifungu ‘tata’ Muswada wa Vyama vya Siasa

Muktasari:

Awali, mvutano ulianza mapema asubuhi wakati wabunge walipokuwa wakichangia na maeneo ambayo yalijadiliwa na wengi ni mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kufuta chama, elimu ya uraia na ruzuku za vyama.


Dodoma. Licha ya juzi Bunge kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, wabunge wengi walihoji vifungu walivyoona vina utata katika muswada huo wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha kifungu kwa kifungu.

Awali, mvutano huo ulianza mapema asubuhi wakati wabunge walipokuwa wakichangia na maeneo ambayo yalijadiliwa na wengi ni mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kufuta chama, elimu ya uraia na ruzuku za vyama.

Vifungu hivyo pia viliibua mabishano kati ya wabunge wa CCM na upinzani.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest alitaka kufanyiwa marekebisho kipengele cha 3 C cha muswada huo ili kisimpe mamlaka msajili kufuatilia na kuchukua hatua kuhusu uchaguzi wa ndani wa vyama na ule wa wagombea, badala yake awe anahudhuria kama mtazamaji.

Akitetea, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Sera), Jenista Mhagama alitaka kifungu hicho kibaki kama kilivyo kwa sababu msajili akiwa mtazamaji hatakuwa na nguvu ya kisheria ya kuchukua hatua endapo atabaini kuwapo kwa ukiukwaji wa sheria hiyo.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa.

Wakati hao wakiunga mkono, hoja ya kutaka kifungu hicho kifanyiwe marekebisho iliungwa mkono na Hamidu Bobali (Mchinga-CUF) na Joseph Selasini (Rombo- Chadema), ambao walisema kikibaki kitamkosesha uhalali msajili wa kusuluhisha migogoro ya uchaguzi na kuongeza gharama kwa Taifa.

Zitto aibua hoja mpya

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe aliibua hoja mpya akisema walikubaliana katika Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kuwa kifungu cha 12 kifutwe kwa sababu kinakwenda kinyume na Katiba, lakini haikufanyika hivyo.

Hata hivyo, mwanasheria mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema Serikali haina taarifa juu ya makubaliano hayo.

Akijibu, Mchengerwa alisema katika maeneo ambayo walikubaliana na Serikali yamefanyiwa marekebisho, lakini hawakuangalia eneo hilo kwa kina na kuwa Serikali imeshatoa ufafanuzi, na wanaafikiana na uamuzi huo.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema katika taarifa ya kamati imependekezwa kufutwa kwa kifungu hicho kuanzia f na g kwa sababu maudhui yake hayaendani na yale ya ibara ya 20(2) ya Katiba ya nchi.

Hata hivyo, Profesa Kilangi alisema vifungu hivyo ambavyo vinaainisha mambo ambayo hayatakiwi kufanywa na vyama havipingani na Katiba.

Lakini mbunge wa viti maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema jedwali la marekebisho lililowasilishwa katika kamati lilionyesha kufutwa kwa kifungu hicho, jambo ambalo wajumbe wote waliridhia.

Malumbano hayo yalisababisha Spika Job Ndugai kumtaka Mchengerwa kulieleza Bunge juu ya jambo hilo na kama walikubaliana na Serikali ifanyie marekebisho.

Akieleza, Mchengerwa alisema kanuni inaitaka kamati kuishauri Serikali na kukubaliana baadhi ya mambo na kwamba inawezekana walishauri, lakini Serikali haikukubaliana nao.

Kauli hiyo ilizua zogo bungeni huku wabunge wengi wakitaka kusimama kuzungumza, lakini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hakuna hata siku moja maoni ya kamati yakawa ni uamuzi wala maoni ya kamati kuwa ndio ya Serikali.

Akihitimisha hoja hiyo, Spika aliwataka wabunge wapige kura na kusema waliokataa kufutwa kwa kifungu hicho wameshinda.

Kifungu cha 26 ambacho kinazungumzia kufutwa kwa chama endapo msajili atabaini kuwa wahusika walitoa taarifa za uongo wakati wa usajili nacho kilizua mabishano, baada ya Zitto kusema walikubaliana katika kamati kifutwe na Serikali, Jumatatu mchana iliwasilisha jedwali la marekebisho kuwa wamekifuta, lakini juzi kilikuwapo.

Alisema pia maoni ya kamati yalitaka kifungu hicho kufutwa kwa sababu msajili atakuwa ameshajihakikishia taarifa za chama husika kabla ya kutoa usajili wa kudumu.

Spika aigeukia kamati

Baada ya kuonekana tena kwa utata wa makubaliano ya kamati na Serikali, Ndugai alisema kamati hiyo inalivuruga Bunge.

“Mnatuvuruga kabisa kamati mnapokuja tofauti na Serikali, na tena kwa kuandika kabisa, maana yake Serikali imekuwa kiburi. Mnapotuandikia hapa mnataka sisi tuwaunge mkono dhidi ya Serikali ambayo haikuwasikiliza kule,” alisema Ndugai.

“Sasa mmeandika nini? Wakati mwingine mjitahidi kuandika vitu ambavyo vina msingi. Maana yake nyie ndio Bunge letu dogo kule.”

Baada ya kupigiwa kura kifungu hicho kilibaki kama Serikali ilivyoamua. Baada ya mvutano muswada huo ulipitishwa na sasa unasubiri saini ya Rais ili kuwa sheria rasmi.