Jinsi wakulima wanavyoibiwa na madalali Dar-2

Monday January 21 2019

 

By Halili Letea, Mwananchi [email protected]

Viongozi wa masoko waliozungumza na Mwananchi wanasema wanatambua uwepo wa madalali katika masoko yao huku baadhi wakisema kuwa watu hao wana umuhimu kwa masoko kwa kuwa ndio wanaowafahamu wateja.

“Tulikuwa na wanunuzi wachache sana kabla ya soko la Buguruni kupunguzwa,” anasema Morocco Milanzi, mwenyekiti wa soko la Buguruni Veternary.

“Madalali ndio waliowaleta wateja wote hawa unaowaona (anaonyesha kwa mkono watu waliokuwa katika harakati za kununua matunda) kwenye soko letu.”

Hata hivyo, Milanzi anakiri kuwepo kwa kesi za kudhulumiwa wakulima na kwamba wamekuwa wakiwafukuza madalali wanaofanya hivyo sokoni hapo, ingawa hana idadi au takwimu za waliofukuzwa. Kwa upande mwingine, anawasifia madalali kuwa ni walipa kodi wazuri na watoaji wa michango ya maendeleo ya soko.

Hali ilivyo katika masoko

Hali katika soko la Temeke Stereo haitofautiani sana na masoko mengine, isipokuwa katika soko hilo kubwa la matunda, viongozi wanatambua kuwa madalali wana vyama vyao kulingana na biashara wanazofanya ambavyo pia vinatambuliwa na uongozi.

Katika soko hilo kila tunda na bidhaa zingine zina viongozi wao na madalali wao.

“Kwa sasa hatuwezi kusema ni madalali kwani wanasaidia watu kuuza na wengine miongoni mwao ni wakulima kabisa,” anasema katibu wa soko hilo, Issa Ndilima.

Baada ya kufuatilia kwa karibu Mwananchi lilibaini kuwa katika masoko takribani yote likiwemo hilo, Ilala, soko la mbogamboga Kigogo Sambusa, wamiliki wa maeneo ya biashara ni madalali ambao huyakodisha au wanapopata wakulima huyatumia kuuzia bidhaa zao. Hali hii imetengeneza ugumu ambao umesababisha wakulima na wauzaji wa kawaida kutolifikia soko moja kwa moja.

Meneja wa soko la Ilala, Selemani Mfinanga anasema anatambua uwepo wa madalali kwenye soko hilo na sheria za soko hilo hazimbagui mkulima wala dalali, akisema jambo muhimu ni kuzingatia taratibu za soko.

Anasema uongozi wa soko hauna utaratibu wa kuingilia makubaliano ya mkulima na dalali wanapokutana kufanya biashara kwani hayo ni makubaliano ya watu wawili.

Udalali wa nafaka

Kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa masoko ya uhakika miongoni mwa wakulima ni sababu mojawapo inayowalazimu kutafuta madalali ambao ndio wanafahamiana na wateja.

Zahoro Mohamedi, mmiliki wa dula la Zanzibar Store lililopo eneo la Temeke Double Cabin aliliambia Mwananchi kuwa madalali huchukua wastani wa Sh20 kwa kila kilo ya nafaka wanayouza kutegemeana na msimu wa mavuno, aina ya nafaka pamoja na uwepo wa bidhaa hiyo sokoni. “Mara nyingi wanachukua kuanzia Sh50 wakati wa mavuno hadi Sh100 kwa kila kilo kipindi mavuno yanapoisha na katika baadhi ya mazao wanachukua Sh20 kipindi bidhaa ikiwepo kwa wingi sokono,” anasema.

Zainabu Mahenge, mkulima wa mahindi kijiji cha Nyang’hwale wilayani Geita anaitaja njia nyingine ambayo madalali wanaitumia kuwa ni pamoja na kuwa na ndoo au madebe ambayo wanayatumia kupimia nafaka.

“Ndoo hizo zimeyeyushwa na zina ujazo mkubwa kidogo ukilinganisha na za kawaida kiasi kwamba ukipima tano tu kwenye gunia moja (kisha ukalipima) unapata kilo 110 na si 100 zinazohitajika.”

Anasema licha ya wao kulifahamu hilo hawana ujanja wa kuwazuia kwani ndio watu pekee wanaoweza kununua mazao yao.

Zainabu ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ushirika cha msingi kijijini kwao kinachoitwa Busambilo Amcos, anasema kukosekana kwa masoko pamoja na maghala ya kuhifadhia nafaka zao kumeendelea kuwatesa.

“Mpaka tunaamua kuuza bidhaa zetu kwa walanguzi,” anasema.

Mwenyekiti wa soko la Temeke, Mohamed Mwekya anasema kwa sasa hakuna madalali katika soko hilo, lakini walikuwepo zamani.

“Waliokuwa madalali ndio hao unaowaona wafanyabiashara walikwishaachana na hiyo kazi muda mrefu,” anasema.

Maombi ya wakulima

Mkulima wa machungwa katika kijiji cha Segera, Ally Salum anasema wanahitaji soko la uhakika la bidhaa zao ili waweze kuuza mazao yao moja kwa moja.

Anasema hata wakiweza kuuza bidhaa moja kwa moja bila kutegemea madalali, bado kumekuwapo na udhaifu wa biashara unaowafanya wapoteze matunda mengi kwa kuoza.

“Siku hizi biashara imekuwa ngumu. Hata kama utabahatika kufika sokoni na kuuza matunda yako mwenyewe wanunuzi hakuna. Angalau Serikali ingeweka viwanda vya usindikaji (mazao) labda vingesaidia kwa kiasi fulani,” anaeleza Salum.

Licha ya kuwapo maeneo mengi nchini yenye maghala ya kuhifadhia mazao yanayosimamiwa na Bodi ya Mamlaka ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), vyama vya ushirika vya msingi (Amcos) na wakulima, wameendelea kulalamikia uwepo wa nafasi finyu za maghala pamoja na miundombinu iliyochakaa inayohatarisha usalama wa mazao yao.

Zainabu anasema, “Msimu unapokuwa vizuri, sehemu ya kuhifadhia mazao yetu inakosekana, lakini pia maghala hayo machache yanavuja na huharibu mazao.”

Pia wanunuzi na wakulima wa mazao ya nafaka wanaitaka Serikali kuwaruhusu kuuza mazao nje ya nchi pale mavuno yanapokuwa makubwa kuliko kutegemea soko la ndani pekee.

Nini kifanyike?

Suluhisho la haraka ambalo viongozi wengi wa masoko wanawashauri wafanyabiashara na wakulima ni kuanza kuuza bidhaa zao kwa mawakala waliosajiliwa na kutambuliwa na Serikali.

Mawakala hao hukusanya mazao kutoka sehemu mbalimbali na kuyahifadhi kwenye maghala ya wafanyabiashara wanaotambulika wanaowatoza wakulima Sh5 kwa kila kilo ya nafaka.

Peter Kata, mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Nafaka Temeke (TGA), anasema kazi yao kubwa ni kuwaunganisha wakulima na wanunuzi watakaonunua mazao bila kuwatoza fedha zozote.

“Mkulima atalipwa kulingana na bei ya soko ya kipindi atapoleta mzigo na sisi tunachukua Sh5 kwa kila kilo,” anasema Kata.

Anasema wanalazimika kuchukua fedha hizo kwa wanunuzi ama mawakala wao kama ada ya uongozi, kulipia tozo na kodi za Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na leseni za biashara.

Zahoro Mohammed ambaye ghala lake liko chini ya TGA, anasema kutokana na kuwepo kwa wakala huo, upatikanaji wa mazao umekuwa nafuu na kero ya madalali imepungua kwa kiasi kikubwa.


Advertisement