Jinsi wanasiasa walivyopokea uamuzi wa Bunge kwa CAG

Wednesday April 3 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Bunge la Jamhuri ya Muungano jana lilipitisha azimio kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ikiwa ni siku sita tangu akabidhi ripoti mpya kwa Rais, ambaye alisema Serikali itaendelea kufanya kazi na ofisi yake.

Uamuzi huo pia umekuja ikiwa imebakia siku sita kati ya siku saba za mwanzo za mkutano wa Bunge. CAG  alimkabidhi Rais John Magufuli ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2017/18 Machi 28 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo unamuweka njiapanda Profesa Assad ambaye ametengwa na Bunge baada ya kusikika katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa akisema kutofuatiliwa kwa ripoti zake ni “udhaifu wa Bunge”.

Pia unaiweka ripoti yake mpya katika sintofahamu baada ya Bunge kusema halitashirikiana naye.

Haijafahamika kama uamuzi huo unamaanisha kuwa Bunge pia halitashughulika na ripoti iliyowasilishwa Machi 28 ya mwaka 2017/18 na hata alipotafutwa kwa simu jana, Spika Job Ndugai hakutaka kuwa bayana.

“Sisi hatufanyi kazi na huyo bwana. Mengine utajumlisha na kutoa wewe kama mwandishi,” alisema Ndugai bila ya kufafanua.

Advertisement

Nje ya ukumbi, mbunge wa Tunduru Kusini (CCM), Daimu Mpakate alisema itakuwa vigumu kwa ripoti ya CAG iliyosainiwa na Profesa Assad kuwasilishwa bungeni ili kujadiliwa.

Uamuzi huo unatupia mpira kwa Rais kuamua hatima ya Profesa Assad kwa mujibu wa Katiba, kwa kuwa Bunge ndicho chombo kinachochambua ripoti zake na kuhoji wahusika na kutoa maelezo kabla ya kutoa maelekezo.

Uamuzi wa jana, ambao ulitangazwa pamoja na ule wa kumzuia mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili, ulifikiwa baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu Profesa Assad na Mdee.

Baada ya kuwasilisha, wabunge walichangia na kupitisha azimio la kutoshirikiana naye katika kikao kilichoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Wakati wakijadili mapendekezo hayo, kuliibuka matukio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuhusisha jambo hilo na sakata la Sh1.5 trilioni lililoibuliwa katika ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 huku mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema naye akirudia kauli ya “Bunge ni dhaifu” wakati akitoa hoja na hivyo Dk Tulia kuagiza naye ahojiwe na kamati hiyo.

“Sisi hapa tunafanya maamuzi ambayo yanaathiri Watanzania,” alisema Mbowe wakati wa mjadala huo.

“Tunataka kupoka haki za msingi za watu kwa sababu sisi tuna mamlaka ya kufanya hivyo.”

Alisema Katiba inatoa haki na uhuru wa mawazo na kila mtu akiwemo CAG, ana uhuru wa kutoa maoni na maelezo bila kujali mipaka ya nchi.

Mbowe alisema kwa mtazamo wa umma kamati hiyo ni ya chama kwa kuwa haina mchanganyiko sawia.

“Natambua kwamba azimio mnalokusudia kulipitisha mahali hapa mmeshalifanyia maamuzi,” alisema Mbowe.

“Historia ambayo mnaiandika leo itawahukumu. Bunge mnajipa utukufu na utukufu ni wa Mungu peke yake. Mnataka kuwaziba Watanzania midomo, watu wasiseme, watu wasi-comment (wasitoe maoni) wakati sisi hapa bungeni tunafanya maamuzi yanawaathiri Watanzania.

“Tunataka kupoka haki za msingi za watu kwa sababu sisi tuna mamlaka ya kufanya hivyo.”

Mbowe alisema Profesa Assad amekaangwa kwa hoja ya Sh1.5 trilioni hadi Sh2.5 trilioni. Alikuwa akirejea sakata la kutoonekana matumizi ya Sh1.5 trilioni katika ripoti ya mwaka 2016/17, jambo lililoibua mjadala mkubwa bungeni.

Ilivyokuwa

Jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu, mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakalasa aliwasilisha ripoti ya sakata la CAG akisema alikiri kutumia neno “udhaifu wa Bunge” lakini hakujutia kauli yake wakati alipohojiwa na kamati hiyo.

“Alipohojiwa na kamati kuhusu maana ya neno udhaifu kwa wananchi wa kawaida na watu ambao taaluma yao siyo wahasibu au wakaguzi alijitetea kuwa yeye alikuwa na maana ya mapungufu na si vinginevyo,” alisema.

Alisema walipotafuta maana ya neno udhaifu kwenye kamusi, walibaini ina maana “isiyokuwa thabiti kiafya, nyonge, yenye kutokuwa na mashiko, goigoi, legevu, hafifu na isiyo imara”.

“Utetezi kuwa akihojiwa alikuwa hakuwa na maana Bunge ni dhaifu, hauna mashiko,” alisema Mwakasaka.

Baada ya kurejea uzoefu wa mabunge mengine pamoja na hatua dhidi ya viongozi wa mikoa, Mwakasaka alisema, “kamati inamtia hatiani Profesa Assad kwa kukiuka kufungu cha 26 (e) cha sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge”.

Wakati Bunge likipitisha azimio hilo, wabunge wa vyama vya upinzani walitoka ukumbini kupinga kitendo hicho.

Akichangia mapendekezo ya kamati hiyo, mbunge wa Chambani (CUF) Yusuf Salim Hussein alihoji: “Mnamtia hatiani kwa kosa gani? Sioni sababu ya kumtia hatiani Profesa Assad.”

Aliwataka wabunge kuacha kujiona kuwa hawana kasoro.

“Sheria ngapi tumetunga ambazo zimekuja na kufanyiwa marekebisho. Mnasema kwanini hakuaga kwa Spika. Kwani alijua atakwenda kuhojiwa na waandishi wa habari?” alihoji.

Advertisement