Jinsi wanasiasa wanavyokuwa vigeugeu nchini

Dar es Salaam. Utaratibu wa mwanasiasa kuhama chama si mgeni, lakini kauli wanazozitoa wakati wakihama zimeonyesha ni vigeugeu na ngeni kwa Watanzania wengi.

Mwanasiasa au raia yeyote wa Tanzania anao uhuru wa kuchagua chama cha siasa anachokitaka kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri.

Hili halikuanza sasa, mwasisi wa Tanu, Chifu Abdallah Fundikira alikihama chama hicho na kujiunga na United Democratic Movement (UMD) alikodumu kuanzia 1993-1999 na kurejea CCM na wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) aliteuliwa kuwa mbunge.

Dk Ndembwela Ngunangwa aliyekuwa mbunge wa Njombe Kusini (CCM) kuanzia 1990-1995, alikihama chama hicho na kujiunga na NCCR-Mageuzi lakini baadaye alirejea CCM.

Hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kauli za ugeugeu wa Chifu Fundikira wala Dk Ngunangwa, walipokihama chama tawala na waliporejea CCM.

Tofauti na wanasiasa hao wa zamani, hivi sasa kumekuwa na kauli za kuhamasisha wafuasi wao wahame pamoja, lakini wanaporejea kwenye vyama vyao vya awali wanakuwa na kauli zinazowaweka njia panda waliowafuata.

Mwananchi imewachambua baadhi ya wanasiasa waliotoka CCM kwenda upinzani na baadaye kurejea katika chama hicho tawala.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni aliyekuwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 alijitokeza kuomba ridhaa ya kugombea urais, lakini chama chake cha CCM kilikata jina lake.

Lowassa hakufurahishwa na uamuzi huo na Julai 28, 2015 alitangaza kujiunga na Chadema akisema CCM haikumtendea haki katika kupitisha majina ya wagombea urais, hivyo hawezi kuendelea kubaki kwenye chama hicho.

“Niliwekewa mizengwe kuhakikisha jina langu halifiki Kamati Kuu na Halmashauri Kuu. Nina nia ya kuleta mabadiliko hivyo kujiunga Chadema ni kuendeleza nia yangu, CCM si baba wala mama yangu, Watanzania kama wameyakosa mabadiliko ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM,” alitamka Lowassa.

Lakini baada ya kudumu kwa siku 1,312 akiwa mwanachama wa Chadema Ijumaa Machi Mosi, 2019, aliamua kurejea CCM. Kabla ya tukio hilo kulikuwa na tetesi kwamba ana mpango wa kurudi CCM, lakini alikanusha madai hayo mara kadhaa akisema hana mpango huo na hajafikiria kuondoka chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Sina mpango wa kuondoka Chadema, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema. Ningetaka kuweka wazi kwa Watanzania na wanachama wa Chadema kwamba sina mpango wa kuondoka Chadema hata kidogo, sina mpango wa kuondoka Chadema, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema.

Ninazo sababu nyingi, katika uchaguzi uliopita (2015) walionibeba ni Chadema na walinibeba tukazunguka na tukapeperusha bendera zetu nchi nzima vizuri na kwa umakini na tukapata watu waliotuamini,” alisema Lowassa katika mahojiano na waandishi wa Mwananchi.

“Watu wale zaidi ya milioni sita ndizo kura wanazokubali Tume ya Uchaguzi, watu wale zaidi ya milioni sita nawaambia nini? Nawaambia naondoka Chadema kwa sababu gani? Kwa hoja gani?” alihoji Lowassa.

Lakini, wiki iliyopita akirejea CCM na kupokelewa katika ofisi ndogo za makao mkuu ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, Lowassa alikuwa na maneno machache kwa kusema, “Nimerudi nyumbani. Bwana Yesu asifiwe, Salaam aleykum, sina mengi; nimerudi nyumbani.”

Mwingine ni James Lembeli aliyekuwa mbunge wa Kahama ambaye Julai 21, 2015 alitangaza kuihama CCM akisema, “Nimekaa nimetafakari na nimezungumza na mama yangu kwa zaidi ya saa 10, mke wangu na watoto wangu, kwa kusikia kilio cha wananchi wa Kahama najiondoa CCM kwa sababu ni chama kilichokithiri kwa vitendo vya rushwa, mizengwe, kukiukwa kwa utaratibu hasa kuelekea uchaguzi.

Hata hivyo, Juni 13 mwaka jana, Lembeli alitangaza kurejea CCM huku akisema amefanya uamuzi huo baada ya mama yake mzazi, Maria Lembeli kumshurutisha hadharani kurejea chama hicho tawala.

Mbali na Lembeli, mwingine ni mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya aliyejiondoa CCM mwaka 2012 akidai hakuna haki wala utawala bora ndani ya chama hicho huku akitangaza kujiunga Chadema iliyompa nafasi ya kugombea ubunge na kushinda kabla ya kujiuzulu.

Lakini, Oktoba 7 mwaka jana, Ole Millya alitangaza kurejea CCM huku akitoa sababu saba miongoni mwa sababu hizo alisema “ni dhahiri kwamba nimepoteza imani na kukosa amani, mahali nilipo sipaoni tena kama ni jukwaa la kunituma na kuhamasisha kuwaletea maendeleo wana Simanjiro.”

Pia, aliyekuwa mbunge wa Sikonge mkoani Tabora, Juma Mkumba ambaye ni mkuu wa wilaya ya Nywang’wale hivi sasa, alihama CCM mwaka 2015 na kwenda Chadema ambako hakudumu kwa muda mrefu.

“Baada ya mtikisiko wa kura za maoni watu wabaya hawakunitendea haki nikaamua kuhamia Chadema kwa muda, nilienda kuwasalimia watani wangu na baada ya kuwasalimia viongozi wa CCM waliniita na kukaa tukazungumza na kuyamaliza,” alisema Mkumba mbele ya Rais John Magufuli mkoani Tabora.

Mwanasiasa mwingine ni Lawrence Masha ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliondoka CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema, lakini baada ya miaka miwili alitangaza kurejea CCM huku akitoa sababu mbalimbali.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini hauna nia wala sababu ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia falsafa, sera na uongozi mbadala. Upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea udhaifu wa CCM badala ya uwezo wake kama mbadala,” alisema Masha wakati huo.