Jokate atamba kupambana na rushwa Kisarawe

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amesema wilaya hiyo imefanikiwa kudhibiti vitendo vya rushwa pamoja na kuzuia watumishi wa umma kuwa na mgongano wa kimasilahi na Serikali

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amesema wilaya hiyo imedhibiti vitendo vya rushwa pamoja na kuzuia watumishi wa umma kuwa na mgongano wa kimaslahi na Serikali.

Akizungumza na watumishi wa umma  wilayani humo leo katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, Jokate amesema tofauti na Serikali zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na rushwa kwa vitendo.

"Mafanikio ya Serikali hii kutatua kero za wananchi yametokana na uadilifu wa watumishi wa umma. Siku za nyuma tulikuwa tukiona watumishi wa umma wakikosa uadilifu, uzalendo na  miradi mingi ilikiwa haikamiliki."

"Sisi tumejikita kutatua changamoto za wananchi, hatuwezi kutatua changamoto hizo bila kuangalia maadili ya watumishi,” amesema.

Kuhusu maadhimisho hayo, Jokate amesema yana lengo la  kuwaelimisha watumishi wa umma juu ya wajibu wao na mipaka yao ya kazi.

Awali, Kamanda wa Takukuru wilayani humo, Alifeo Silungwe amewataka watumishi wa umma kujiepusha na mgongano wa kimaslahi kwa kuwa ndiyo chanzo cha rushwa.