Jukwaa la Wahariri lamshauri Nape kuhusu Bunge Live

Nape Nnauye 

Muktasari:

Katibu wa Jukwaa la Wahariri, Neville Meena amesema Nape alipoingia madarakani aliamua kuendeleza mazuri na mabaya yaliyokuwa katika mchakato wa Sheria ya Haki ya kupata Habari


Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limemshauri aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuunganisha nguvu ya pamoja na wadau wa habari katika harakati za kudai matangazo ya Bunge live.

Katibu mkuu wa jukwaa hilo, Neville Meena amesema bado TEF kwa kushirikiana na wadau wanaendelea na madai ya kurejesha urushaji wa matangazo ya Bunge live, hivyo kwa nafasi yake itaongeza ushawishi katika kufanikisha harakati hizo.

Meena ameitoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 19, 2019 ikiwa ni siku moja baada na Nape kunukuliwa katika mahojiano na kipindi cha Clouds 360, kinachorushwa na Clouds TV, akisema si yeye aliyeanzisha ajenda ya kuua matangazo hayo bali ilikuwapo tangu Bunge la 10.

Aprili 25, 2016 jijini Dodoma, akiwa waziri mwenye dhamana, Nape alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akitetea hoja ya Serikali ya kutorusha matangazo ya Bunge moja kwa moja live.

“Kauli yake inaongeza uzito katika harakati hizo kwamba aliyekuwa kinara hata kama hakukiri moja kwa moja lakini ameona yale yalikuwa ni makosa, lakini sasa aungane na wadau wengine kwa sababu ana nafasi ndani ya Bunge,” amesema Meena.

Amesema akiwa waziri mwenye dhamana, Nape ambaye ni mbunge wa Mtama (CCM) aliona ni jambo sahihi kwa wakati huo.

Katika hatua nyingine Meena alimtupia lawama Nape akisema wakati anaingia madarakani aliamua kuendeleza mazuri na mabaya yaliyokuwa katika mchakato wa Sheria ya Haki ya kupata Habari.

“Anachokifanya Nape ni kukimbia lawama, kwa hiyo uwezo wa kukubali au kukataa (kuzima Bunge) ulikuwa mikononi mwake, hata kama si yeye binafsi alikuwa na uwezo wa kushawishi, kuonyesha athari za kuzima matangazo hayo, tulikutana naye kwenye vikao lakini ni miongoni mwa watu waliokuwa na misimamo mikali,” alisema Meena.