KAMPENI: Magufuli apiga ‘push-up’ nne

Wednesday September 23 2015

Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli

Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli akipiga ‘push up’ kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Changarawe Kayanga Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera jana. Picha na Adam Adam Mzee wa CCM 

By Peter Elias, Mwananchi

Kagera. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana alirukaruka na kupiga ‘push up’ nne mbele ya wananchi wa Karagwe ili kuthibitisha kwamba ana nguvu za kufanya kazi.

Akiwa katikati ya hotuba yake, Dk Magufuli alifanya zoezi hilo na kushangiliwa na watu waliohudhuria mkutano huo huku akisisitiza kuwa ana nia, nguvu na uwezo wa kuwatumikia Watanzania na hatabadilika akipata nafasi hiyo.

“Kuna watu wanasema ‘people’s power’ (nguvu ya umma), basi wanipe hiyo power (nguvu) kwa sababu nina power ya kufanya kazi, si mnaona ninaweza hata kurukaruka?” alisema mgombea huyo huku akirukaruka juu na wananchi wakizidi kumshangilia.

Dk Magufuli aliwahoji wananchi kama watampa kura baada ya kuwaonyesha kuwa ana nguvu, kabla wananchi hawajamjibu, mgombea huyo akauliza tena, ‘...au mnataka nijaribu kupiga push up hapa?’ Wananchi wakajibu ‘piga’.

Mgombea huyo alianza kupiga ‘push up’ hizo huku akishangiliwa na wananchi, kisha aliendelea na hotuba yake na kusema hiyo ndiyo sifa ya rais ajaye na kusisitiza kuwa yeye anatosha kwa nafasi hiyo.

Ingawa hakutaja chama, Dk Magufuli alikuwa anailenga Chadema inayoungwa mkono na Ukawa, ambayo hutumia kaulimbiu ya ‘Peoples’s Power’.

“Ninatambua shida zenu watu wa Karagwe, likiwamo suala la soko la kahawa yenu. Ninawaahidi kwamba mkinichagua nitahakikisha bei ya kahawa inapanda ili watu wa Uganda waanze kuleta kahawa yao hapa,” alisema.

Mgombea huyo wa CCM alifanya kampeni zake katika majimbo ya Karagwe, Nkenge, Kyerwa na Ngara. Akiwa Karagwe, alianza kwa kumnadi mgombea ubunge, Innocent Bashungwa, jambo ambalo ni tofauti na anavyofanya katika majimbo mengine kwa kutambulisha wagombea baada ya kuhutubia.

“Ninawaomba sana ndugu zangu, nichagulieni huyu kijana, baba yake Mzee Bashungwa niliwahi kufundisha naye shule moja kule Sengerema. Kwa hiyo, namjua vizuri kijana huyu, msiniangushe watu wa Karagwe,” alisema.

Alisisitiza kuwa endapo watamchagua, atajenga kilomita tano za barabara kwa lami katika mji wa Karagwe. Aliahidi pia kujenga barabara ya Karagwe – Benako yenye urefu wa kilomita 100.

Mgombea huyo aliahidi kushughulikia fidia za wananchi waliobomolewa nyumba zao wakati wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Misenyi. Alisema atahakikisha kuwa wananchi wote wanaostahili, wanalipwa fidia.

“Mnipe kura nikamalize tatizo hili, bahati nzuri tuna Waziri (William) Lukuvi ambaye ni mchapa kazi pale wizara ya ardhi, anajua matatizo haya,” alisema.

Akiwa Nkenge, Wilaya ya Misenyi, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk Diodorus Kamala alimwomba Dk Magufuli kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa Kakunyu na kusaidia ujenzi wa barabara ya kutoka Bunazi mpaka Kagera Sugar kwa kiwango cha lami. Dk Kamala aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo: “...Ninatambua changamoto zote za hapa, naomba mnichague ili tushirikiane katika kukabiliana na changamoto tulizonazo,” alisema mgombea huyo ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.

Mkazi wa Misenyi, Baraka Mushumbusi alisema kero kubwa kwao ni kodi nyingi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Alisema wanapokwenda kununua bidhaa Uganda, wanatozwa kodi mbili ndani ya Tanzania pekee.

“Tukichukua bidhaa kutoka Uganda tunalipa kodi kwa URA (Mamlaka ya Mapato Uganda) na tukifika hapa tunalipa kodi nyingine mpakani na huku ndani, hii imekuwa ni kero kwetu, tunaomba wapunguze kodi,” alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulambo alisema kulikuwa na vizuizi 200 katika Wilaya ya Misenyi lakini vimepunguzwa mpaka kufikia 50 ambavyo alisema bado ni vingi.

Advertisement