KCB yakuza mtaji wa wanawake wajasiriamali

Muktasari:

  • Ni katika mkakati wa kuhakikisha inawaandaa wateja wapywa watakaoendelea kuhudumiwa nayo na kupambana na umasikini.

Dar es Salaam. Benki ya KCB imetoa Sh85 milioni kwa  wanawake 17 kuwasaidia kukuza biashara zao.

Fedha hizo ambazo kila mmoja amepata Sh5 milioni ni muendelezo wa program ya tujiajiri inayoendeshwa na benki hiyo tangu mwaka 2016 ikilenga kuwahamasisha wanawake wajasiriamali kutumia huduma za benki kukuza biashara zao.

Kwa miaka mitatu ya uwepo wa program hiyo, mkuu wa idara ya masoko na uhusiano wa KCB, Christine Manyenye amesema zaidi ya wanawake 800 wamenufaika na mafunzo yanayotolewa hivyo kuendesha biashara zao kisasa zaidi.

“Hii ni awamu ya pili. Tutatoa sh5 milioni kwa wanawake 17 wenye biashara tofauti. Tunaamini kiasi hiki kitasaidia kuimarisha biashara za wajasiriamali hawa,” amesema Christine.

Kabla ya kutoa fedha kwa wajasiriamali ambao ni sharti wawe na akaunti KCB, wataalamu wa benki hiyo huwapa mafunzo ya namna ya kufanya biashara kwa namna bora zaidi kwa nadharia na vitendo.

Katika awamu ya kwanza mwaka huu, wanawake 256 walishiriki mafunzo ya darasani yaliyowaongezea maarifa ya utunzaji wa vitabu vya kumbukumbu, masoko na urasmishaji wa biashara. Miongoni mwao, 115 walipata mafunzo ya vitendo kwenye maeneo hayo matatu.

Fedha wanazopewa wanawake wanaoshiriki program hiyo, ni mpango maalumu, hawatakiwi kuzirudisha ingawa benki hiyo hufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha zinatekeleza malengo ya kukuza uchumi wa muhusika.

Benki ya KCB ni miongoni mwa taasisi kongwe ya fedha Afrika Mashariki. Ilianzishwa 1896 visiwani Zanzibar kabla haijasambaa kwenye nchi sita inakoto ahuduma hivi sasa ikiwamo Tanzania, Kenya, Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na Ethiopia.

Katika nchi hizo, KCB iliyoorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Nairobi (NSE) na Rwanda (RSE) ina jumla ya matawi 262, mashine 962 za kutolea fedha (ATM) na mawakala 15,000.