Kabila, Tshisekedi wakutana kujadili uteuzi wa waziri mkuu

Muktasari:

  • Viongozi hao ambao awali walikuwa wapinzani wamekutana kuzungumzia suala la uteuzi wa waziri mkuu, huku ikiwa imetimia miezi minne tangu Rais Felix Tshisekedi achaguliwe kuongoza nchi hiyo

Kinshasa,DRC. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi amekutana na Rais mstaafu, Joseph kabila kuzungumzia suala la uteuzi wa waziri mkuu.

Marafiki hao walikutana Jumatatu wiki hii na kuzungumzia kuhusu nafasi ya waziri mkuu ambayo imebakia  wazi, ikiwa ni miezi minne baada ya uchaguzi wa urais uliompa ushindi Tshisekedi.

Awali, Tshisekedi na Kabila walikuwa hawaelewani kufuatia mvutano wa kisiasa lakini baada ya uchaguzi wawaili hao waliamua kufanya kazi kwa ushirikiano wakiwa katika muungano mmoja wa kisiasa.

Rais Tshisekedi na Kabila walikuwa hawajakutana kwa wiki kadhaa kutokana na ziara za kikazi za Tshisekedi. Lakini kwa pande zote mbili wanahakikisha kuwa Rais wa sasa na mtangulizi wake huzungumza mara kwa mara.

Kuhusu suala la waziri mkuu, mazungumzo yanaendelea karibu miezi minne baada ya  Tshisekedi kuapishwa kuwa Rais. Mwanzoni wawili hao walikuwa wamechagua timu za mazungumzo, lakini mazungumzo yao hayakuwa na mafanikio.