Kabila aandaliwa kugombea urais 2024

Muktasari:

  • Wasimamizi wa vyama wote wametakiwa kuwa waaminifu kwa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila

Kinshasa, DRC. Rais mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Joseph Kabila amekutana na wawakilishi wa Muungano wa vyama tawala chini ya utawala wake, FCC, shambani kwake katika kijiji cha Kingati.

Moja ya mambo yaliyozungumzwa katika mkutano huo ni kuangalia namna ya kumfanya Kabila agombee na kushinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao ambao huenda ukafanyika mwaka 2024 au 2025.

Kwa upande wake Kabila katika mkutano huo ametoa mwelekeo mpya wa chama hicho baada ya aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya FCC, Emmanuel Shadary kushindwa kupata kiti cha urais katika uchaguzi wa Desemba 30 mwaka uliopita.

Akizungumza wakati wa mkutano huo mratibu wa FCC, Nehemie Mwilanya, amewaambia wasimamizi wa vyama hivyo kuwa mpango mpya uliopo ni kukubali kuwa waaminifu kwa Kabila na kuheshimu maelekezo yote ya FCC.

Katika hatua nyingine mratibu huyo pia amesema lengo kuu kwa sasa ni kumuandalia Kabila mazingira ya kuchaguliwa tena kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi utakaoandaliwa baada ya muhula huu wa miaka mitano.

Taarifa kutoka makao makuu ya chama hicho cha FCC imesema Februari 22, Kabila atakutana na wabunge wote wa muungano huo waliochaguliwa.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa hivi karibuni wa DRC, baadhi ya wachambuzi wa siasa walizungumzia uwezekano wa Kabila kuwania tena kiti cha Urais katika uchaguzi ujao.