Kagame asema Rwanda haitapigana na Uganda

Muktasari:

Rais wa Rwanda, Paul Kagame amepuuza uwezekano wa nchi yake kuingia vitani na Uganda, ingawa amesisitiza kuwa nchi hiyo jirani inafadhili waasi wa nchi yake.

Kampala. Rais wa Rwanda, Paul Kagame amepuuza uwezekano wa nchi yake kuingia vitani na Uganda, ingawa amesisitiza kuwa nchi hiyo jirani inafadhili waasi wa nchi yake.

Kagame amesema hayo katika mahojiano na Gazeti la Taz la Ujerumani, wakati wa mkutano wa kimataifa jijini Brussels, Ubelgiji na kunukuliwa na The Daily Monitoe la Uganda.

Katika majibu yake kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi katika uhusiano wa nchi hizo jirani, Kagame alisema “Watu wanahofia vitana baina yetu (Uganda na Rwanda). Sioni kama kuna vita vinakuja kati yetu, nadhani Uganda inajua gharama zake. Hatutaki kwenda chini katika njia hiyo kwa kuwa kila mmoja atapoteza kitu,” alisema.

Kagame ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliongeza, “Tumeona Uganda ikihusika katika kufadhili vikundi vya waasi vyenye silaha dhidi yetu kwa sababu wanadhani hatuangalii maslahi ya Uganda. Hawatambui kwamba Rwanda ina serikali tofauti na ingependa kulipa wekwa kwao, hilo tu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu onyo la vita alilolitoa kwa Uganda Aprili, Rais Kagame alijibu: “Ndiyo, (vita vitatokea) ikiwa utavuka mpaka.

Unaweza kufanya chochote unachotaka ndani ya himaya yako, kama kukamata watu. Lakini ukivuka mpaka wetu na kutaka kufanya mambo ndani ya himaya yetu – hicho ndicho nilichomaanisha.”

Rwanda imekuwa inaituhumu Uganda kwa kuwakamata watu wake na kuwashikilia wakati mwingine ikiwa kimya na bila kuwafungulia mashtaka, jambo ambalo Kagame alilieleza gazeti la Ujerumani kuwa halikuwa zuri.

Alisema Uganda ingelitumia sheria zake kumshtaki Mnyarwanda yeyote anayekamatwa badala ya kuwashikilia kwa muda mrefu kwa madai ya kuifanyia ujasusi na baadaye kuwaachia.

“Lakini ukamataji ni wa jumla, wanakamata wanawake, wanaume, vijana na hata wanafunzi kutoka shuleni. Mara ya mwisho nilipokutana na )Rais wa Uganda) Museveni nilisema hizo tuhuma hazina mashiko. Watu 200 walikuwa wamekamatwa na hawakumshtaki hata mmoja. Hilo linaonyesha ukubwa wa tatizo.

Mwezi uliopita, Museveni na Kagame walikaa jirani jijini Pretoria wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Viongozi hao walionekana kwenye televisheni wakizungumza muda wote wa sherehe hizo. Haifahamiki kama wakati huo ndipo walijadili masuala yanayohusu nchi zao.

Mapema mwezi huu, Rwanda ilifungua mpaka wake kwa ajili ya magari ya mizigo kutoka Uganda kwenda Kigali, uliokuwa umefungwa tangu Februari, lakini wananchi wake waliendelea kuzuiliwa kuingia Uganda.